Baraza la Umoja wa Ulaya (EU) limeonya kuhusu matokeo ya hatua ya Marekani ya kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) yenye makao yake The Haugue nchini Uholanzi.
Taarifa ya baraza hilo imeeleza kuwa, uamuzi wa Marekani wa kuiwekea vikwazo Mahakama ya ICC kutokana na kutoa hati za kukamatwa kwa Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel na aliyekuwa waziri wake wa vita Yoav Gallant utakuwa na matokeo mabaya.
Antonio Costa Mkuu wa Baraza la Ulaya ameonya kuwa kuwekewa vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ni tishio kwa uhuru wa taasisi hiyo na kunavuruga muundo wa haki za kimataifa.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya amesema hayo, baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutia saini dikrii (amri ya utendaji) ya kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa kile alichokiita uchunguzi usio na msingi dhidi ya Marekani na Israel, kuhusu mauaji ya kimbari huko Gaza.