WANAYANGA hivi sasa wanatamba baada ya kuishusha Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara hali inayoongeza presha ya kubeba ubingwa.
Hayo yakijiri, kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davids anawavutia kasi huku akisema ngoja waone itakuwaje hadi mwisho kwani hata wao mbio za ubingwa bado zipo katika mafaili yao.
Simba ambayo imetoka kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Fountain Gate katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Februari 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara, keshokutwa Jumanne ina kibarua cha kuikaribisha Tanzania Prisons.
Sare hiyo imewafanya Simba kubaki nafasi ya pili kwenye msimamo na pointi 44 ikizidiwa moja na Yanga huku zote zikicheza mechi sawa 17. Kabla ya hapo, Simba ilikuwa na nafasi kubwa ya kurejea kileleni baada ya kukaa hapo kwa muda mrefu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu ambaye ameiongoza Simba kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, amesema kinachoendelea kwenye ligi ni kitu cha kawaida hivyo suala la wao kubeba ubingwa lipo palepale.
Fadlu ana imani kwamba msimu huu ataanza safari ya kurudisha makombe ya ligi ndani ya Simba baada ya kuyakosa kwa misimu mitatu mfululizo yakibebwa na watani wao Yanga.
“Ligi bado ina mechi nyingi, kwa hiyo lolote linaweza kutokea, ngoja tuone mwisho wa safari itakuwaje.
“Suala la kufanya makosa kwenye mchezo wa soka kila mmoja linaweza kumtokea, kikubwa tunataka kurudi kwenye njia yetu ya ushindi.
“Simba itarudi kileleni na bado tuko hai kwenye mbio za ubingwa licha ya kufanya makosa ya kuangusha pointi mbili za kwanza ugenini msimu huu,” alisema kocha huyo raia wa Afrika Kusini.
Mara ya mwisho Simba kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara ilikuwa msimu wa 2020–2021 wakati ikifundishwa na Kocha Didier Gomes Da Rosa. Ubingwa huo ulikuwa wa nne mfululizo na ilikuwa 2017–2018, 2018–2019, 2019-2020 na 2020–2021.
Katika hatua nyingine, kocha huyo amesema baada ya mchezo alikaa na kiungo wake Ladack Chasambi na kujaribu kumuweka sawa baada ya kujifunga bao ambalo liliinyima Simba pointi tatu baada ya kuwa mbele.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Fadlu alisema, amekaa na kuongea na mchezaji wake na kumwambia makosa yaliyofanyika ni ya kawaida kwenye mchezo wa mpira wa miguu.
“Ukiangalia kabla ya kosa hilo kulikuwa na makosa mengi, pia Ladack alikuwa na mchezo bora kwani ndiye aliyetengeneza nafasi ya bao la kwanza. Hivyo Chasambi asilaumiwe, mashabiki wakumbuke yeye ndiye alisaidia kupatikana bao letu,” alisema Fadlu.
Jumanne Februari 11 mwaka huu Simba itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa KMC Complex kuikaribisha Tanzania Prison kutoka Mbeya ukiwa ni mwendelezo wa Ligi Kuu Bara ambapo inaweza kurejea kileleni endapo itashinda kisha watani zao Yanga watakaocheza kesho Jumatatu watapoteza au kutoka sare dhidi ya JKT Tanzania ugenini.