Feitoto kafichua kitu miasisti yake

KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amefichua kasi yake ya kutengeneza mabao haitapoa kwani ana malengo makubwa zaidi msimu huu.

Fei Toto ambaye tayari amevunja rekodi ya asisti zilizowekwa msimu uliopita na Kipre Junior aliyekuwa akiitumikia Azam kabla ya msimu huu kutimkia MC Alger ya Algeria na alikuwa nazo tisa, amesema kwa sasa bado hajafika anakopataka.

Kiungo huyo wa zamani wa Yanga, msimu uliopita alimaliza na asisti saba akifunga mabao 19 nyuma ya kinara wa mabao Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyefunga 21.

Hadi sasa katika raundi ya 17, Fei Toto ndiye kinara wa asisti akiwa nazo 10 huku akifunga mabao manne. Kinara wa mabao ni Clement Mzize wa Yanga mwenye tisa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fei Toto alisema kitendo cha kufikisha asisti 10 kwake ni kitu kizuri kwani ni mara ya kwanza kinatokea kwenye maisha yake ya soka la ushindani.

Alisema baada ya kufikisha asisti 10, anataka zifike 15 akiwa na imani zitaisaidia timu yake kufikia malengo waliyojiwekea kwani wana washambuliaji wanaozitumia vizuri pasi zake za mwisho.

“Nafurahi kuona nimevunja rekodi ya asisti mapema kukiwa na mechi nyingi bado za kucheza, nimempita Kipre Junior aliyeibuka kinara wa asisti msimu uliopita.

“Malengo yangu nataka kuweka rekodi kubwa zaidi kwa kufikisha asisti 15, kwa kuwa bado timu yangu ina mechi nyingi za kumaliza msimu naamini jambo hili litawezekana,” alisema Fei Toto ambaye huu ni msimu wa pili anaichezea Azam.

Wakati Fei Toto akiyasema hayo, kocha wake, Rachid Taoussi alisema: “Feisal ni mchezaji mzuri mwenye kipaji kikubwa na anaweza kucheza nafasi nyingi, ila mimi napendelea kumtumia kama namba 10.

“Namba anayoichezea inamfanya aweze kutumia ubora wake na kutengeneza nafasi, lakini haina maana nimemzuia kufunga, jambo muhimu kwanza ni atengeneze nafasi kwa wenzake na kufunga akiweza.”.

Related Posts