Msaidie hivi mtoto kukabiliana na hisia

Sauda (39) ni mama wa Rahma (11) anayesoma darasa la sita.

Rahma, pamoja na kuwa na uwezo mkubwa darasani, ana tabia ya kulia bila sababu za msingi.

Mara nyingi hushitaki wenzake kwa makosa madogo, ambayo kwa mujibu wa mama yake, angeweza kuyashughulikia bila kulazimika kusema.

Mbali na tabia hiyo ya kudeka, Rahma ana shida ya kulipuka kihisia. Katika michezo, kwa mfano, Rahma aghalabu hupandwa na hasira kiasi cha kuweza kuwashambulia wenzake kwa makonde na maneno makali.

Sauda alichukulia tabia hii kuwa ya kawaida. Lakini kadiri Rahma anavyoendelea kukua, hali hii inaendelea kumtia wasiwasi. Katika mazungumzo yetu, ninagundua Rahma ana tatizo la uchanga wa kihisia.

Mtoto mwenye uchanga wa kihisia ana uwezo mdogo wa kudhibiti hisia zake. Mbali na kushindwa kuishi vizuri na watu, anaweza kushindwa kushirikiana vizuri na wenzake darasani, hali inayoweza kuathiri maendeleo yake kimasomo, pia kujidhuru kiafya na hata kisaikolojia.

Mtoto wa namna hii anapokutana na mazingira yanayomkatisha tamaa, mathalani, humwia vigumu kukabiliana nayo arudi katika hali yake ya kawaida.

 Je, mzazi unawezaje kumsaidia mtoto kuwa mkomavu kihisia, unaweza kumpa uwezo wa kujitambua na kuwa mlinzi wa hisia zake mwenyewe? Hapa tunaangazia masuala kadhaa.

 Uchanga wa kihisia unachangiwa na malezi yanayowanyima watoto fursa ya kutambua hisia zao. Kwa kujua kuwa hisia fulani hazikubaliki, watoto hujifunza kuficha na kukana hisia zao ili wawe salama.

 Hali hii ina hasara kubwa mbili. Kwanza, inajenga tabia ya kuwategemea watu wengine kulinda hisia zao. Wanapojisikia vibaya wanafikiri kuna mtu mwingine amefanya wajisikie vibaya na wao hujiondoa kwenye wajibu.

Lakini pili, inajenga mazoea mabaya ya kuhukumu watu wengine wanapoonyesha hisia zisizotarajiwa.

Hisia ni maumbile. Mfundishe mtoto kuzitambua na kuzikubali. Mtoto ajue tofauti ya kufurahi, kukasirika, kukereka, wasiwasi, huzuni, hofu na hisia nyingine. Kutambua hisia zake kutamsaidia kujielewa anapokuwa katika hali fulani. Katika mazingira ambayo wewe kama mzazi umemruhusu kuzionyesha, mtoto hatajisikia hatia kuzikubali.

 Uchanga wa kihisia, kwa upande mwingine, unachangiwa na tabia ya kuwalaumu watu wengine kwa hisia anazokuwa nazo mtoto. Ongea na mtoto aelewe kuwa hisia alizonazo ni zake. Hana mtu mwingine wa kumlaumu anapokuwa na hisia fulani. Hasira, huzuni, kukata tamaa, wasiwasi, havisababishwi na mtu mwingine, bali yeye mwenyewe.

 Mtoto anahitaji kufahamu kuwa vile tunavyojisikia ni matokeo ya vile tunavyofikiri. Hasira, huzuni, furaha vyote vinaanzia kwenye mawazo yetu. Namna gani tunatafsiri mambo ndiyo hasa chanzo cha hisia tulizonazo.

Mtoto anapofahamu uhusiano huu kati ya fikra zetu na hisia tunazokuwa nazo, unakuwa umemsaidia kuwajibikia zaidi hisia zake. Hatakuwa mwepesi kumlaumu mtu mwingine pale anapojisikia vibaya kwa sababu ataelewa kilichomfanya ajisikie vibaya si mtu mwingine tafsiri yake ya mambo.

 Ruhusa ya kuonyesha hisia zake

 Kuna nyakati sisi kama binadamu tunakuwa na huzuni. Mioyo yetu inaweza kuomboleza, kusikitika, kuhuzunika kwa sababu kuna mambo fulani tusiyoyatarajia yametokea kwenye maisha yetu.

 Hisia hizi zina faida kwetu. Tunapoomboleza, tunajipa matibabu ya nafsi. Mtu anayeomboleza anajisaidia kukabiliana na kile kilichotokea na anajiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kurejea kwenye hali ya kawaida baada ya muda mfupi.

 Mtu asiyejipa muda wa kuomboleza mara nyingi anajizuia kukubali hali halisi. Mtu huyu huchukua muda mrefu kurejea kwenye hali yake ya kawaida. Wakati mwingine anaweza kupata shida ya matatizo ya nafsi kwa sababu hakuipa nafsi nafasi ya kucheua.

 Ni muhimu wazazi kuwafundisha watoto kutoa hisia zao, hasa zile hasi. Mtoto anapokasirika, anaposikitika, usimkemee kumfanya aamini kuwa hasira ni kitu kibaya. Somo muhimu analolihitaji mtoto ni kuchunga kile anachokifanya akiwa amekasirika.

 Mfundishe kukabiliana na hisia

 Hisia ni maumbile. Hatuwezi kuhukumiwa kwa kuwa na hisia fulani. Changamoto, hata hivyo, ni vile tunavyovifanya tunapokuwa na hisia fulani.

 Ili uweze kumfundisha mtoto kudhibiti hisia zake, hatua ya kwanza ni wewe mwenyewe kuelewa hisia mbalimbali. Nikuulize, kwa mfano, hisia zipi kati ya hizi unakumbuka kuzipitia juma hili? Hasira, furaha, wasiwasi, faraja, furaha, wasiwasi, masikitiko, huzuni, kukerwa? Ulichukua hatua gani kukabiliana na hisia hizo?

Kuna mbinu nyingi unazoweza kuzitumia unapokuwa kukabiliana na hisia zako mfano kupumzika mahali palipotulia; kusoma kitabu; kuangalia televisheni; kupooza hasira kwa kufanya utani; kushiriki michezo; kuongea na mtu mwingine.

 Kupitia tabia zako mwenyewe mfundishe mtoto namna ya kukabiliana na hisia zake kwa kutumia njia sahihi. Kufoka, kupigana, kutafuta wa kumlaumu si mbinu muafaka

Related Posts