Zijue ishara hatari za kimaadili kwa mtoto

Malezi ya mtoto yanahitaji uangalizi wa karibu. Mzazi makini anaweza kutambua mabadiliko madogo yanayoashiria mtoto anaanza kupotoka kimaadili na kuchukua hatua mapema.

Hali hii unaweza kuibaini kama utakuwa na mawasiliano mazuri, usimamizi wa karibu na ushirikiano na walezi wengine.

Hivyo kama atakuwa anaanza kutumbukia katika nyendo zisizo salama, mzazi unaweza kumsaidia mtoto wako kuepuka njia mbaya na kurudi katika mwenendo mzuri.

Malezi ya mtoto ni jukumu nyeti linalohitaji uangalifu mkubwa kutoka kwa mzazi. Watoto hukua katika mazingira yanayowakabili na wakati mwingine, huweza kuathirika kwa njia hasi.

Hivyo mzazi makini anaweza kutambua dalili za awali za mtoto anayeanza kupotoka kimaadili na kuchukua hatua stahiki kabla hali haijawa mbaya zaidi.

Leo nimeona tujadili ishara za mabadiliko na hatua za haraka ambazo mzazi anaweza kuchukua kumrejesha mtoto katika njia sahihi.

Baada ya kuzungumza na wataalamu, wanasema mtoto ambaye alikuwa mchangamfu na mtii ghafla anakuwa mkimya, hasikii anachoambiwa au anaonyesha ukaidi wa hali ya juu, mzazi anapaswa kutambua kuwa hiyo inaweza kuwa dalili kuwa mwanawe anapitia mabadiliko yasiyofaa.

Lakini pia ukibaini mtoto anapoteza msukumo wa kusoma, kushiriki kazi za nyumbani, au kutojali maadili aliyofundishwa, mzazi anatakiwa kufuatilia nyendo zake.

Mtaalamu mwingine aliniambia endapo mtoto anaanza kujihusisha na marafiki waovu, wakiwemo wale wanaotumia lugha chafu, wavivu au wenye mienendo mibaya, kuna uwezekano mkubwa naye akawa ameanza kukengeuka kimaadili.

Wakati mwingine, mwanao ambaye hukutarajia kumuona akizungumza lugha chafu, kubishana na mzazi au kuonyesha tabia ya dharau, basi huenda anapitia ushawishi wa nje wenye athari mbaya, hivyo anapaswa kudhibitiwa mapema.

Tukumbuke kuwa mtoto anayekosa utulivu nyumbani na anayetafuta kila mara nafasi ya kutoka nje bila sababu ya msingi, naye pia anaweza kuwa na mambo yasiyofaa anayoyafanya nje ya usimamizi wa wazazi.

Lakini pia mtoto anayeficha mambo, hasemi ukweli au anayejihusisha na vitendo vya ajabu naye anaweza kuwa kwenye njia ya kupotoka, hataki kwenda kanisani au msikitini, mzazi chukua hatua.

Unawezaje kuidhibiti hali hiyo?

Ili kudhibiti hali hiyo kwa haraka, mzazi unatakiwa hatua ya haraka ya kuzungumza na mwanao kwa upendo badala ya kumkemea kwa ukali.

Mweleze madhara ya mienendo anayojihusisha nayo. Mazungumzo ya kirafiki yanaweza kufungua njia ya kuelewa kinachomsumbua.

 Ikiwezekana mzazi aanze kufuatilia tabia ya mtoto wake, marafiki anaoshirikiana nao na maeneo anayoyatembelea. Hili linaweza kusaidia kugundua chanzo cha tatizo mapema.

Ni muhimu mzazi kuweka mipaka inayojulikana kwa mtoto, ikiwa ni pamoja na muda wa kutoka nje, matumizi ya simu na mitandao ya kijamii sambamba na shughuli za muda wa ziada.

 Lakini pia ushirikiano baina ya mzazi na walimu wake shuleni, mzazi unaweza kupata taarifa zaidi kuhusu mwenendo mzima wa mtoto awapo shuleni.

Nasema hivyo kwa sababu mtoto anapokuwa na muda mwingi wa ziada, anaweza kujihusisha na makundi mabaya.

Hivyo mzazi anaweza kumshawishi kushiriki katika michezo, shughuli za kijamii, au mafunzo yanayomjenga kimaadili.

Kwa sababu mara zote watoto huiga tabia za wazazi wao. Mzazi anapaswa kuonyesha tabia ya maadili kwa vitendo ili mwanawe aige tabia hizo.

 Ikiwa mzazi amejitahidi lakini bado anashindwa kudhibiti hali hiyo, wataalamu wa malezi hushauri apelekwe kwa mshauri wa saikolojia au mtaalamu wa malezi kwa msaada wa kitaalamu.

Related Posts