Na Mwandishi Maalum,Tunduru
WAKAZI wa kijiji cha Ligunga Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma,wameanza kuwa na matumaini ya kupata huduma ya maji safi na salama baada ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira(Ruwasa),kuwa katika hatua za mwisho kukamilisha mradi wa maji ya kisima utakaohudumia wakazi 4,242 wa kijiji hicho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa Ligunga wamesema,hatua ya Serikali kujenga mradi huo umewapa faraja kubwa ya kuondokana na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama iliyokuwepo kwa muda mrefu.
Sada Mshamu, mradi huo utakuwa mkombozi mkubwa hasa kwa akina mama na watoto ambao kila siku wanatembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji yanayopatikana mbali na makazi yao.
Mshamu alisema,ukosefu wa maji ya uhakika umechangia sana kurudisha maendeleo nyuma,kwa sababu wanatumia muda mrefu kwenda kuchota maji mtoni au kukaa kwenye mabomba ya kupampu kwa mkono,hivyo wanashindwa kufanya shughuli mbalimbali za kujikomboa na umaskini.
“katika kijiji chetu kuna wazee ambao hawawezi kusukuma pampu kwa ajili ya kupata maji kutokana na kuishiwa nguvu,lakini mradi huu utakapokamilika utasaidia kumaliza changamoto ya maji iliyopo kwa muda mrefu katika kijiji chetu”alisema Mshamu.
Mkazi mwingine wa Ligunga Yusuf Yasin alisema,huduma ya maji ni kero ya muda mrefu na imechangia sana kurudisha nyuma maendeleo ya kijiji hicho kwani wanatumia muda wao mwingi kwenda kutafuta maji badala ya kujikita katika shughuli za kiuchumi.
Alisema,kuna mabomba machache ya kupampu yaliyojengwa tangu miaka ya tisini,hata hivyo yanawaathiri kiafya kwani wanatumia nguvu kubwa kusukuma maji na watu wasiokuwa na nguvu wanakwenda mtoni au kununua maji yanayouzwa kati ya Sh.1,000 na 2,000 kwa ndoo ya lita.
Kaimu Mtendaji wa kijiji cha Ligunga Shija Ndeleba alisema,Viongozi wa kijiji hicho wanatumia muda wao mwingi kusuluhisho migogoro ya mara kwa mara ambayo chanzo ni kugombea maji na ameiomba Ruwasa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya mradi huo ili Wananchi wapate huduma ya maji kwenye maeneo yao na viongozi wajikite kwenye kusimamia shughuli za maendeleo.
Mhandisi wa Maji kutoka Ofisi ya Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Tunduru Felix Kakele alisema,katika mwaka wa fedha 2024/2025 wamepanga kutekeleza program ya visima 10 ambavyo vitahusisha uchimbaji na ujenzi wa Miundombinu ya kusambaza Maji kwa Wananchi ikiwemo katika kijiji cha Ligunga.
Alisema,Wilaya ya Tunduru imepata visima 10 vitakavyogharimu Sh.milioni 600,kati ya hivyo visima 9 vimechimbwa na viko katika hatua mbalimbali za ukamilisha ikiwemo mradi wa kisima cha Ligunga.
Alisema,gharama hizo zinahusisha uchimbaji wa visima,ujenzi wa kioski,ununuzi wa vifaa na malighafi za ujenzi ambazo ni matofali,sementi,nondo,mabomba na mfume wa umeme jua(Solar Power).
“Hii miradi imekwenda maeneo ya vijijini,kwa hiyo tunafunga mfumo wa umeme jua ili kurahisisha uendeshaji na kupunguza gharama kwa Wananchi kwa sababu kiwango cha uchangiaji wa huduma ya maji itakuwa chini,vifaa vyote kwa ajili ya kutekelezaji miradi hiyo vimefika na kuanza kutumika”alisema.
Alisema,lengo la Serikali kufikisha asilimia 85 ya utoaji wa huduma ya maji ifikapo mwaka 2025 kwa Wananchi wa maeneo ya vijijini,lakini Ruwasa Wilaya ya Tunduru imefikisha asilimia 83 na miradi hiyo itakapokamilika utaongeza asilimia 3.5 hivyo kufikisha asilimia 86.6 ifikapo Mwezi Desemba mwaka huu.
Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia fedha Ruwasa Wilaya ya Tunduru ili kutekeleza miradi ya visima 10 na miradi mingine inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali.
Baadhi ya Wakazi wa kijiji cha Ligunga kata ya Ligunga Wilayani Tunduru wakipata huduma ya maji kutoka kwenye bomba la kupampu kwa mkono ambalo ndiye tegemeo pekee kwa Wananchi wa kijiji hicho kupata huduma ya maji safi na salama,hata hivyo Serikali kupitia RUWASA imeanza kuchimba kisima kirefu ili kukabiliana na kero hiyo Muonekano wa kituo mojawapo cha kuchotea maji kilichojengwa katika kijiji cha Ligunga Wilayani Tunduru na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA) kwa ajili ya kutoa huduma ya maji safi na salama kwa Wananchi wa kijiji hicho.
Baadhi ya Wakazi wa Kijiji cha Ligunga Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma,wakims ikiliza Afisa Uhusiano wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma Geddy Ndimbo aliyenyoosha mkono kulia,baada ya wakazi hao kutembelea ujenzi wa kituo cha kuchotea maji kinachojengwa kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya maji safi na salama.