Magata apania rekodi Mtibwa Sugar

KIUNGO mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Fredrick Magata amesema anajisikia fahari kucheza ndani ya kikosi hicho msimu huu, huku akiweka wazi mojawapo ya malengo yake makubwa ni kuweka rekodi ya pili maishani mwake ya kuipandisha timu Ligi Kuu.

Nyota huyo anayeitumikia timu hiyo kwa msimu wa pili sasa tangu ajiunge nayo akitokea Mbeya Kwanza, alisema ushirikiano uliopo baina yao, viongozi na benchi la ufundi, anaamini watatimiza malengo waliyojiwekea.

“Moja ya rekodi ninayotaka kuiweka ni kuipandisha Ligi Kuu Mtibwa Sugar kama nilivyofanya wakati nikiwa na Mbeya Kwanza msimu wa 2021-2022, naamini inawezekana kwa sababu ukiangalia hadi sasa hatupo sehemu mbaya ya kutimiza hayo,” alisema.

Magata aliyechangia mabao 13 ya timu hiyo msimu huu hadi sasa kati ya 31, akifunga mawili na asisti 11, alisema ushindani ni mkubwa sana hasa raundi ya pili, ila watapambana bila ya kujali kuhusu wapinzani wao.

Mtibwa iliyocheza michezo 17, kabla ya ule wa jana dhidi ya Mbeya City, imeshinda 14, sare miwili na kupoteza mmoja tu, safu ya ushambuliaji imefunga mabao 31 na kuruhusu saba, ikiwa kileleni mwa msimamo wa Championship na pointi 44.

Related Posts