ACHANA na beki Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ wa Yanga kuingia kambani mara nne akiwa ni beki pekee mwenye mabao mengi Ligi Kuu, kuna kiraka Novatus Miroshi wa Goztepe ya Ligi Kuu ya Uturuki (Süper Lig) anafanya balaa.
Kwenye Ligi Kuu Bara, Bacca amefunga mabao hayo manne akiisaidia Yanga, huku pia akiufanya ukuta wa mabingwa hao watetezi kutokuruhusu mabao ikifungwa machache (saba), kiwango chake kikiendana na Miroshi ambaye amekuwa na wakati mzuri akiwa na Goztepe.
Nyota huyo ambaye pia ana uwezo wa kucheza kiungo wa chini amekuwa na muendelezo mzuri sio tu wa kuzuia lakini hata kufunga na kuisaidia timu hiyo.
Kwenye Ligi hiyo ambayo pia Jose Mourinho anafundisha akiwa na Fenerbance ambayo aliwahi kupita Mtanzania Mbwana Samatta, Novatus amefunga mabao matatu na kuruhusu ukuta wake kufungwa mabao 27.
Kitendo cha kupata namba kwenye kikosi hicho kinathibitisha uwezo mkubwa alionao na ukomavu anaoendelea kuupata kwenye ligi kubwa Uturuki na kuwa miongoni mwa nyota wa Kitanzania walioweka rekodi ya kufunga wakiwa na timu za Ulaya kama ilivyokuwa kwa Samatta aliyepita klabu mbalimbali.
Nyota huyo hana ubingwa wa Ligi Kuu Bara lakini ana ubingwa wa Ligi Kuu Ukraine akiwa na Shakhtar Donetsk ikiwa ndio taji lake la kwanza na kucheza michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa mchezaji wa pili kufanya hivyo.
Kabla ya hapo Miroshi alicheza ligi mbili tofauti Ulaya, Ligi Kuu Israel akiwa na Maccabi Tel Aviv na Ligi ya Ubelgiji akiwa na Zulte Waregem.