KIUNGO wa Cosmopolitan, Gilbert Boniface amesema kikosi hicho kwa sasa kinapitia kipindi kigumu kutokana na kutokuwa na mwenendo mzuri katika Ligi ya Championship, licha ya kukiri wachezaji kijumla wanajitoa kuipigania timu yao.
Kauli ya nyota huyo inajiri baada ya timu hiyo kushinda michezo miwili tu kati ya 17 hadi sasa, ikitoka sare miwili na kupoteza 12 ikishika nafasi ya 15 na pointi tisa, hivyo kujiweka katika mazingira magumu ya kujinasua kutoka mkiani.
“Ni mwenendo mbaya sana lakini ninachokiona tunakosa morali tu kwa sababu tunapambana ila tunajikuta tunapoteza michezo kirahisi, hatupo sehemu nzuri sana, hivyo ni lazima tupambane kujinasua na janga la kushuka daraja.”
Akizungumzia msimu huu, Gilbert alisema umekuwa mgumu kutokana na ushindani uliopo, lakini kikosi hicho bado kina nafasi ya kujinasua ikiwa kitapambana katika michezo yote iliyobakia ya mzunguko wa pili.
“Ligi imekuwa ngumu sana kwa sababu kila timu ina wachezaji bora na wazoefu, ukiangalia hapa kwetu wengi wetu ni wapya na hatujakaa pamoja kwa muda mrefu, kwa michezo ya hivi karibuni inatupa mwanga ingawa tuna kazi kubwa ya kufanya pia.”