KIUNGO Mtanzania, Charles M’Mombwa anayekipiga Newcastle Jets ya Australia taratibu anaanza kuingia kwenye kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu ya nchini humo.
Huu ni msimu wake wa kwanza nyota huyo kuichezea Newcastle lakini sio mgeni wa ligi hiyo kwani hapo awali aliichezea Macarthur FC kwa misimu minne kuanzia msimu 2020/24.
Ikiwa raundi ya 18 ya ligi, timu hiyo imecheza mechi 15 ikiwa nafasi ya 11 kwenye msimamo na pointi 15, ikishinda mechi nne, sare tatu na kupoteza nane.
Kiungo huyo alisajiliwa hivi karibuni akitokea Macarthur FC ya nchini humo na amecheza mechi tatu akiitumikia Newcastle kwa dakika 71.
Mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Perth Glory zilizotoka sare ya 2-2 na M’mombwa akicheza dakika 30, dhidi ya Central Coast Mariners sare 2-2 akicheza dakika 24 na Melbourne Victory, chama lake likishinda mabao 3-0 akimaliza dakika 17 akiwa hana bao hadi sasa.