KOCHA wa Maafande wa Polisi Tanzania, Mussa Rashid amesema moja ya malengo aliyopewa ni kuhakikisha timu hiyo inamaliza nne bora ‘Top Four’, na wanahitaji sapoti zaidi kutoka kwa mashabiki na viongozi ili kufikia hilo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mussa alisema wachezaji wengi waliopo katika kikosi hicho ni wapya na ameanza majukumu yake kwa muda mfupi wakati timu ikiwa imeanza mashindano, hivyo itachukua muda kidogo ingawa sio mbaya zaidi.
“Nimekuja katika changamoto mpya na tayari nimepewa malengo hayo ambayo lazima niyapambanie, natambua ni ngumu kutokana na ushindani uliopo, naamini tukiendeleza ushirikiano tutatimiza kwani gepu la pointi na waliokuwa juu yetu sio kubwa.”
Timu hiyo imecheza michezo 17, kabla ya ule wa jana dhidi ya Kiluvya United na imeshinda mitano tu, sare mitano na kupoteza saba, ikiwa nafasi ya 10 na pointi 20, huku ikipambana kurejea Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2022-2023.
Kocha huyo wa zamani wa African Sports na Green Warriors, amejiunga na kikosi hicho akitokea Biashara United ya Musoma na ameungana kikosini na Bernard Fabian aliyeanza nacho msimu huu, ingawa kwa sasa ameteuliwa kuwa msaidizi wake.