Dk Magoma wa Chadema afariki, Lissu kuongoza mazishi Jumanne

Hanang’.  Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Manyara, Dk Derick Magoma, amefariki dunia leo, Jumapili, Februari 9, 2025, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu.

Dk Magoma, enzi za uhai wake, aligombea ubunge wa Hanang’ kwa tiketi ya Chadema katika vipindi viwili, mwaka 2015 na 2020. Hata hivyo, alishindwa na wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa lo Jumapili, Februari 9, 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Aman Golugwa, imeeleza kuwa Dk Magoma alifariki dunia akipatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

Golugwa amesema mazishi ya Dk Magoma yatafanyika Jumanne, Februari 11, 2025, katika mji wa Magugu, Kijiji cha Matufa, Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara na kwamba Mwenyekiti wa Chadema-Taifa, Tundu Lissu, atawaongoza wanachama wa chama hicho kushiriki safari ya mwisho ya Dk Magoma hapa duniani.

Amesema kuwa leo saa 10:00 jioni, mwili wa Dk Magoma utaagwa Hospitali ya Muhimbili, kisha kuanza safari ya kuelekea Arusha. Mwili huo unatarajiwa kufika Arusha alfajiri ya kesho, Jumatatu,  na kisha utapelekwa nyumbani kwake (Kimandolu) kwa ajili ya waombolezaji kuaga kuanzia saa 7 mchana.

Golugwa ameongeza kuwa baada ya kuaga mwili huo, safari ya kuelekea Magugu, mkoani Manyara, itaanza saa 11 jioni.

Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Katesh wamemlilia Magoma, aliujekuwa mchangiaji wa maendeleo kupitia mitandao ya kijamii. Mkazi wa mji mdogo wa Katesh, Gifufana Gafufen, amemuelezea marehemu Magoma kama mtu aliyekuwa anapenda maendeleo.

“Amepambania sana kile anachokiamini, kawaida shoka linalotumika kukata miti mingi mikavu na migumu huisha haraka, ila ameacha alama yake. Sisi tutaishia kusema R.I.P kwa sababu mwisho kufikiri kwetu,” amesema.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) wa Mkoa wa Manyara, Asia Halamga, amesema Dk Magoma alikuwa rafiki wa wengi, mstaarabu na muungwana.

Mkazi wa Kata ya Ganana, Simon Kimario, amesema ili kumuenzi Magoma, kila kijiji na kaya ipate maji safi na salama.

 “Vizuri havidumu mbele yetu, nyuma yako nakukumbuka sana ulivyokuja matangarimo na maji kwenye chupa tofauti tofauti ukitutetea raia juu ya maji tunayokunywa. Hatimaye mabomba yamefika kila kijiji,” amesema.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema, kupitia akaunti yake ya X, ameweka picha ya Dk Magoma na kuandika: “Ni siku mbaya sana kwangu kuandika meseji hii, kwamba rafiki yangu na mpiganaji na mwenyekiti mstaafu wa Mkoa wa Manyara kwa chama chetu amefariki akiwa anatibiwa katika Hospitali ya Muhimbili. Derick Magoma alikuwa mtu mwema na mpiganaji sana. Natoa pole kwa familia yake, ndugu, jamaa na marafiki.”

Kada wa CCM aliyewahi kuwa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa, pia kwenye akaunti yake ya X ameweka picha ya Dk Magoma na kuandika: “Umeondoka mapema sana kaka, nimebaki midomo wazi! R.I.P Magoma.”

Related Posts