WAKATI Ligi ya Wanawake ikisaliwa na mechi sita, Ligi ya Mkoa nayo ikitarajiwa kuanza, Ukerewe Queens ambayo kwa sasa inaitwa Tausi FC imefanya usajili wa maana kujiandaa na ligi hiyo ikiwaleta ndugu zao nyota wa Yanga, Djigui Diarra na Stephane Aziz KI.
Ukerewe ambayo ilikuwa inashiriki Ligi ya Mkoa wa Mwanza imenunuliwa na kampuni ya Tausi na sasa rasmi itaitwa Tausi FC ikitoka mkoani humo na kuweka kambi Dar es Salaam.
Inaelezwa mipango ya timu hiyo ni kupanda daraja kucheza Ligi Kuu ya Wanawake msimu ujao na ili ifanikiwe imeanza kufanya usajili mbalimbali wa kimataifa na ndani.
Mmoja wa viongozi wa Tausi FC (jina tunalo) aliliambia Mwanaspoti malengo ya timu hiyo ni kupanda daraja msimu ujao ili kupata uzoefu wa ligi hiyo.
“Soka la wanawake linakuwa sana hivyo tumeamua kuwekeza kwenye eneo hilo na tunaamini tukipanda daraja tutajiandaa vyema, kupitia timu yetu wachezaji watapata nafasi ya kuandaliwa vyema kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa nje,” alisema kiongozi huyo.
Hadi sasa timu hiyo imetambulisha wachezaji wanne wa kimataifa, Adama Congo mshambuliaji raia wa Burkina Faso, Adiaratou Coulibaly na Fatoumata Diara wote ni manahodha wa timu ya taifa ya Mali na kipa Ruth Aturo kutoka Uganda.
Ukiachana na usajili wa kimataifa pia wametambulisha nyota wazoefu wa ndani akiwemo Madeline Otieno ambaye aliwahi kucheza Simba Queens, Fountain Gate Princess na Mashujaa Queens, Fatuma Yahaya aliyepita Allan Queens na Masala Queens.
Khadija Hussein beki kiraka aliwahi kupita katika klabu mbalimbali ikiwemo Alliance Girls, Kigoma Sisters na Baobab Queens, Golikipa Khadija Thadeo alipita Tanzanite Queens, Ruvuma Queens, Ilala Queens na Ceasiaa Queens na Jacqueline Joseph winga wa kulia, winga wa kushoto na kiungo mshambuliaji aliwahi kupita Yanga Princess.
Timu hiyo pia imemtambulisha Kocha Mkuu, Maria Ruiz kutoka Hispania ambaye aliwahi kucheza klabu kama Real Madrid ya wanawake akisaidiana na Hilda Masanche ambaye ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya vijana Tanzania pia imemtambulisha kocha wa kipa, Alloy Agu kutoka Nigeria.