Mwanza. Ukiiona utasema ni Meli ya ‘MV Lady Jean’, kwa waumini na viongozi wa Kanisa la Afrika Inland Church of Tanzania (AICT), hiyo ni hospitali inayotembea kwa lengo la kufikisha huduma ya matibabu kwa wakazi wa visiwa vilivyoko ndani ya Ziwa Victoria.
Uzinduzi wa meli ya MV Lady Jean ulifanyika jana Jumamosi Februari 8, 2025, ukiongozwa na Askafu Mkuu wa AICT, Mussa Magwesela, ukishuhudiwa na mamia ya waumini na wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Meli hiyo yenye urefu wa Mita 15 na upana mita nne, ina uwezo wa kubeba watu zaidi ya 10 wakiwamo watoa huduma ya Afya (madaktari bingwa) na wahudumu wa meli ambao kazi yao itakuwa kusogeza huduma ya matibabu ya kibingwa na kibingwa bobezi kwa wakazi wa visiwani.
Meli hiyo itaungana na meli nyingine mbili zinazotumika kama hospitali inayotembea ikiwamo meli ya MV Jubilee Hope inayomilikiwa na AICT na MV Salim inayomilikiwa na Taasisi ya Christian Life World Mission ya jijini Mwanza.
Meli zote zinatoa huduma ya matibabu katika visiwa zaidi ya 80 vilivyoko ziwa Victoria.
“Huu mwaka ni wa 112 tangu (AICT) tumeanza kutoa huduma za Afya kule Kolandoto. Tuliona kuna haja ya kuanza kutoa huduma za afya visiwani, tulienda kazungumza na Wizara ya Uchukuzi na Afya wakatusaidia kuanza kutoa huduma hizo,” amesema Askofu Magwesela.
Magwesela amesema meli hiyo ya MV Lady Jean imenunuliwa (bila kutaja gharama) na AICT kwa ushirikiano na Mgodi wa Madini Geita (GGML), Vine Trust na Serikali kupitia Bohari ya Dawa nchini, MSD.
Kuhusu utoaji wa huduma hizo kwa kipindi cha miaka 12, Askofu huyo amesema kupitia meli ya MV Jubilee Hope inayotimiza miaka 10 ya kutoa huduma katika visiwa hivyo, imefanikiwa kutoa matibabu kwa wakazi wa visiwani zaidi ya 450,000.
“Huduma za kimatibabu zilizotolewa kwa kipindi hicho ni pamoja na kumuona Daktari, vipimo vya maabara na Dawa kwa wagonjwa wapya na wanaojirudia, hii inadhihirisha athari chanya ya kazi yetu katika jamii ya watanzania,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema kuanzishwa kwa huduma ya afya visiwani kupitia meli hizo siyo tu kunasogeza huduma kwa wakazi wa visiwani, pia kunapunguza muda na gharama ambazo wakazi wa maeneo hayo wangetumia kufuata matibabu maeneo ya nchi kavu.
“Uwepo wa meli ya MV Jubilee Hope na uzinduzi wa MV Lady Jean kutasaidia kutoa matibabu kwa maelfu ya watanzania wanaoishi visiwani ambako kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma hizo,” amesema Mtanda.
Amesema kupitia huduma za hospitali zinazotembela (meli hizo), Serikali imeshuhudia kupungua kwa magonjwa, kuokoa maisha ya wagonjwa na kuboresha ustawi wa afya wa jamii ya visiwani.

Meli ya ‘MV Lady Jean’ itakayokuwa ikitoa huduma ya matibabu kwa wakazi wa visiwa vilivyo ndani ya Ziwa Victoria. Meli hii imezinduliwa na Kanisa la AICT.
“MV Jubilee Hope iliwafikishia matibabu zaidi ya watu 500,000, katika kipindi cha miaka 10, ikiwemo utoaji wa chanzo, matibabu ya Malaria, uzazi, upasuaji mdogo na matibabu ya kinywa na meno. Uzinduzi wa MV Lady Lean ni hatua nyingine ya kuwafikia watanzania wengi zaidi visiwani,” amesema Mtanda.
Makamu wa Rais wa Mgodi wa GGML, Simon Shayo amesema ujio wa meli hiyo ni jitihada za kampuni kurejesha kwa jamii na kusaidia uboreshaji wa huduma na ustawi wa jamii.
“Tutaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha ustawi wa jamii unaimarishwa na tunaamini meli hizi zitatumika ipasavyo kusogeza huduma kwa wakazi wa visiwani ambao wanapitia changamoto ya huduma ya Afya kutokana na umbali,” amesema Shayo.
Akizungumzia ujio wa meli ya MV Lady Jean, Mkazi wa Kisiwa cha Kome Wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Alexander Shimiwa amesema anaamini maisha ya wajawazito na wanaopatwa magonjwa ya dharura yanaenda kunusuriwa.
“Visiwani kuna changamoto kubwa pamoja na jitihada za Serikali kufikisha huduma za afya Ila bado kuna maeneo hazijafika ipasavyo. Meli hii huenda ikaleta matumaini mapya kwetu wakazi wa visiwani,” amesema Shimiwa.