DABI ya watani wa jadi inayowakutanisha Simba na Yanga itapigwa Machi 4 baada ya mapumziko ya siku 30 ya Ligi. Dabi hiyo ya Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) inapigwa siku nne tu kabla ya watani hao kwa upande wa wanaume kukutana Siku ya Wanawake Duniani, Machi 8 Kwa Mkapa, Dar es Salaam.
Ligi ya Wanawake imesimama kwa siku 30 kupisha kalenda ya FIFA kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) ambayo fainali itapigwa nchini Morocco, kuanzia Februari 17 hadi 26 na Tanzania ikianza na Equatorial Guinea Februari 20 kufuzu WAFCON 2026.
Mapumziko hayo yanahusisha kwa timu za Simba, JKT na Yanga Princess ambazo zimetoa wachezaji wengi kwenye kikosi cha timu ya taifa huku ligi hiyo ikiendelea kwa baadhi ya timu ambazo zina viporo.
Ligi itakaporejea utashuhudiwa mchezo wa dabi kati ya Yanga Princess na Simba Queens Machi 4, kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam.
Hii ni mara ya tatu kwa timu hizo kukutana msimu huu baada ya nusu fainali ya ngao ya jamii ambayo Yanga iliitoa Simba kwa mikwaju ya penati 5-4 baada ya sare 1-1 na duru la kwanza la Ligi Simba ikawatandika wananchi mabao 2-0.
Mnyama anaendelea kushikilia kileleni kwenye mechi 12 ikifunga mabao 43 na kuruhusu saba ikiwa na pointi 34, huku Yanga ikiwa nafasi ya tatu na pointi 24 baada ya michezo 11.
Hadi sasa Simba na JKT ndizo ambazo hazijapoteza michezo yao ligi kuu, Wanamsimbazi hao ikitoa sare moja sawa, huku wanajeshi wao ikiwa na sare mbili na kushinda michezo yote.