Ushirikiano wa manispaa ya Moshi, Mji  wa Marburg Ujerumani wazaa matunda

Moshi. Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, imepokea gari moja la zimamoto na uokoaji kutoka Jiji la Marburg nchini Ujerumani, ambalo litasaidia katika kukabiliana na majanga ya moto ambayo yamekuwa yakitokea maeneo mbalimbali katika Manispaa hiyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji leo Jumapili Februari 9, 2025, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo amesema waliahidiwa magari mawili ya zimamoto na sasa limekuja moja, ambalo litasaidia shughuli za uokozi wakati wa majanga ya moto.

Amesema ushirikiano wa miji hiyo miwili inahusisha ushirikiano katika sekta ya afya, tiba, kinga na majanga ya mamoto.

“Oktoba 25, 2023, marafiki zetu kutoka Ujerumani walitutembelea hapa Moshi, tuliwaeleza changamoto zetu zinazotukabili ikiwemo upungufu wa gari la zimamoto na uokoaji, wenzetu hawa walituahidi wakirudi Ujerumani watatusaidia kutupatia magari mawili, na leo wametuletea gari moja, na tumeambiwa lingine liko kwenye mchakato” amesema Kidumo.

Ameongeza:”Marburg ni mji uliojikita kwenye masuala ya elimu zaidi, hususani ile inayohusiana na afya, tiba na kinga, na katika kupambana na majanga eneo la uokoaji hasa zimamoto hivyo uhusiano huo utasaidia kupata vifaa vya zimamoto pamoja na elimu juu ya uokoaji na kupamabana na majanga.”

Aidha, Meya ametaka jeshi la zimamoto na uokoaji kulitunza gari hilo ili kuweza kudumu na kusaidia kukabiliana na majanga ya moto kwa muda mrefu.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe amesema walilazimika kuomba kupatiwa gari la zimamoto, baada ya Manispaa ya Moshi kuwa na majanga mengi ya moto, huku jeshi la zimamoto likiwa na upungufu wa magari ya ukoaji.

“Tulilazimika kuomba gari hili kwa rafiki zetu wa Ujerumani baada ya kuona tuna majanga ya moto ikiwemo lile lililotokea katika Soko la Mbuyuni, na wenzetu wa jeshi la zimamoto wamezidiwa na mkoa ni mkubwa na magari ni machache,” amesema Nasombe

Kwa upande wake,  Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo, ameushukuru uongozi wa Manispaa ya Moshi kwa kuendelea kujenga uhusiano mzuri wa ushirikiano kati ya mji hiyo miwili, ambayo matunda yake wanayaona.

Amesema soko la Mbuyuni liliungua mara mbili na kutokana na kukosekana kwa gari kwa jeshi la zimamoto na uokoaji, walilazimika kuomba gari kutoka kiwanda cha TPC, hivyo kupatikana kwa gari hilo kutaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za uokozi wakati wa majanga ya moto.

“Tunawashukuru sana wadau wetu Marburg, haya ni matokeo ya hoja binafsi ya kushawishi halmashauri ziweze kushirikiana na Jeshi la zimamoto na uokoaji katika kuwahudumia wananchi”amesema Mbunge Tarimo.

Naye Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro Mkaguzi Jeremiah Mkomagi, ameushukuru uongozi wa Manispaa ya Moshi kwa namna ambavyo wamekuwa na ushirikiano  na Jiji la Marburg.

Related Posts