Mitazamo tofauti ya wadau kuhusu mapigano DRC

Dar es Salaam. Ingawa hatua zilizotangazwa na wakuu wa nchi baada ya kikao chao cha kumaliza mgogoro Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zinatajwa kuwa muhimu kwa sasa, wadau wamesema mustakabali wa amani ya Taifa hilo, utaamuliwa na uimara wa jeshi lake yenyewe.

Sambamba na hilo, wadau hao wamesema njia nyingine ya utatuzi wa mgogoro huo wa miongo kadhaa nchini humo, ni kutafutwa mzizi wake na anayedai haki ili apewe, anayelalamikia kunyanyaswa aachwe huru.

Lakini wengine wanaona hatua ya kukutana kwa wakuu wa nchi ni muhimu na hata maazimio yaliyofikiwa yataleta ahueni ya mgogoro unaoendelea.

Hoja hizo zinakuja siku moja baada ya wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kukutana jijini Dar es Salaam nchini Tanzania kujadili suluhu ya mgogoro wa miongo kadhaa kati ya vikundi vya waasi kikiwamo cha M23 dhidi ya DRC.

Kwa sauti moja wakuu hao wa nchi, waliokutana Dar es Salaam, waliazimia kusitishwe mapigano, huku wakiwataka wakuu wa majeshi ya ukanda wa maziwa makuu kukutana ndani ya siku tano na 30 kwa mawaziri wa kisekta wa ukanda huo.

Licha ya hatua hizo muhimu, baadhi ya wadau wameibua wasiwasi, pengine zisizae matunda tarajiwa, wakirejea mikutano kadhaa ya wakuu wa nchi na makubaliano, lakini hayakufanikiwa kumaliza mgogoro huo.

Miongoni mwa mikutano iliyoonekana kuikaribia suluhu ya mgogoro huo ni ule wa Machi 23, mwaka 2004 uliohusisha wakuu wote wa nchi za ukanda huo na kuazimia suluhisho la vita vya DRC lifanywe kwa kumhusisha kila mdau.

Sambamba na hilo, mkutano huo uliazimia mahitaji ya vikundi vya waasi ikiwamo kupewa haki kama raia wengine  DRC na wale wenye uwezo wa kijeshi waingizwe jeshini, yote hayakutekelezwa na mapigano yakaendelea.

Kwa sababu ya kushindikana kwa hatua zote hizo, wadau hao wa diplomasia na siasa za Afrika wamesema hakuna jipya litakalofanyika ikiwa mengi yalifanywa bila muafaka kupatikana, huku wakionyesha njia ya kumaliza mgogoro huo DRC kama Taifa huru, ijiimarishe kulinda mipaka na watu wake.

Uimara uanze na DRC yenyewe

Kwa mtazamo wa Balozi Liberatha Mulamula aliyewahi kuiongoza sekretarieti ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa mwaka 2004, kuna umuhimu wa mageuzi katika kila kitu likiwamo jeshi nchini DRC.

Kwa sababu DRC ni nchi huru na yenye hadhi, amesema ina wajibu wa kulinda mipaka, heshima na wananchi wake na hakuna mwingine wa kulitekeleza hilo kwa niaba yake.

“Nchi lazima isimame kama Taifa lililo huru, liweze kusimama kama nchi, liwe na jeshi linaloweza kulinda nchi yao, hakuna nchi yoyote inayoweza kukulindia nchi,” amesema Balozi Mulamula ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa.

Amesema umefika wakati nchi za Afrika ziwe na mifumo imara ya kiutawala badala ya kuanza kuilaumu au kuitegemea jumuiya ya kimataifa.

Balozi Mulamula amesema jeshi la DRC lina wanajeshi zaidi ya 100,000 na wakiamua wenyewe bila msaada wa yeyote, linawezekana kumaliza kinachoendelea ndani ya siku moja.

“Tukiamua kuisaidia DRC katika kulifunza jeshi lao likasimama inawezekana, lakini tunaamini katika njia ya maridhiano na mazungumzo,” amesema.

Amesema tatizo la DRC halipaswi kuangaliwa kwa jicho moja, ni muhimu zitumike njia zote zinazowezekana kumaliza mgogoro unaoendelea.

‘Utatuzi uanzie kwenye mzizi’

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo amesema hatima ya mgogoro huo, itapatikana kwa kutatua mzizi wake.

Dk Masabo amesema mzizi wa machafuko DRC ni Serikali ya nchi hiyo kutowakubali baadhi ya watu wake kuwa raia wake tangu enzi za uhuru.

Ameeleza baada ya mipaka ya ukoloni kulikuwa na watu waliokuwa wanaishi katika ardhi ya DRC waliotambulika kuwa Banyamulenge.

“Serikali ya DRC, mara kadhaa imedai si raia wake na inawataka warudi nchini Rwanda ilhali si nchini mwao,” amesema Dk Masabo.

Katika mazingira hayo, amesema ndipo raia hao walipogeuka kuwa vikundi vya waasi na wanapingana na Serikali yao tangu uhuru wa Taifa hilo.

Dk Masabo amesema  suluhisho la mgogoro huo ni DRC kuwapa hadhi ya uraia Banyamulenge na kuwatambua kama raia wao.

Amesema hilo ndilo lililoazimiwa Machi 23, 2004 na wakuu wa nchi za ukanda wa maziwa makuu, lakini hayakutekelezwa na ndio sababu ya kuzaliwa Kikundi cha Waasi cha M23.

“Kwa hiyo hatima ya mgogoro ipo mikononi mwa DRC wenyewe wakubali kuwapa hadhi ya uraia wenzao na watengeneze utaratibu wa kushughulikia matatizo ya enzi za ukoloni,” amesema Dk Masabo.

Mbali na mtazamo wa Dk Masabo, Msomi wa Siasa za Afrika, Ezekiel Kamwaga anaona ilikuwa lazima wakuu wa nchi za SADC na EAC kukutana kwa sababu kinachoendelea Mashariki mwa DRC kinawaathiri pia.

Tofauti na hatua za mwaka 2004, Kamwaga amesema mkutano wa sasa mbali na kukubaliana kumaliza mgogoro kwa njia ya kidiplomasia, lakini umetoa nafasi kwa wakuu wa majeshi kupanga namna ya kusimamisha mapigano yanayoendelea.

“Wamekubaliana kuumaliza mgogoro kwa njia ya diplomasia, lakini tayari kuna watu wenye bunduki waliopo kwenye mgogoro. Kwa kawaida watu wenye bunduki aghalabu huwa na heshima kwa wenye bunduki wenzao.

“Kitendo cha kuwataka wakuu wa majeshi wakutane kwanza kusimamisha bunduki na kumaliza uhasama ni hatua muhimu na nzuri kuwahi kufanyika,” amesema Kamwaga ambaye pia ni mwandishi mwandamizi nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Kamwaga, wakuu wa majeshi wana nafasi nzuri ya kusimamisha kinachoendela, kwa sababu haitoshi kuuondoa mgogoro wa kijeshi kwa njia za kisiasa na kidiplomasia pekee.

Mwanazuoni huyo anayaona maazimio ya kikao hicho, yanaweza kuwa hatima ya mgogoro huo hasa pale yalipofungua milango kwa jumuiya ya kimataifa ambayo si sehemu ya EAC na SADC kuongeza nguvu ya kuisaka suluhu.

“Pamoja na nia njema, lazima jumuiya ya kimataifa iwe sehemu ya kuisaka suluhu ya changamoto inayoendelea kwa sababu EAC na SADC pekee haitakuwa na nguvu ya kifedha kugharimia vikosi vya kuzuia mapigano iwapo watakubaliana kuvipeleka DRC,” amesema Kamwaga.

Hata hivyo, amesema nchi za magharibi kwa sasa zimegawanyika, jambo linalotoa nafasi nzuri kwa viongozi wa Afrika kukubaliana namna ya kushirikiana na kila mmoja ili kumaliza kinachoendelea.

Mtazamo wa Kimwaga unashabihiana na tamko la Jukwaa la Asasi za Kiraia Ukanda wa Maziwa Makuu, lililoeleza hatma ya mgogoro huo ni kusimamiwa kwa kilichokubaliwa na wakuu wa nchi kwenye kikao chao cha Dar es Salaam.

Kenney Walusala ambaye ni mmoja wa viongozi wa jukwaa hilo, amesema hatua ya wakuu hao wa nchi kuwataka wakuu wa majengo wa kikanda kukutana ndani ya siku tano ili kukomesha mapigano ni muhimu.

Si hivyo tu, ameeleza hata hatua ya kuwakutanisha mawaziri wa kikanda ndani ya mwezi mmoja itakuwa na tija katika kuufikia muafaka wa mgogoro unaoendelea.

Ingawa kuna makubaliano hayo, Walusala amesema jambo la kuzingatiwa ni utekelezwaji wa kila azimio kama yalivyowekwa katika kikao hicho cha wakuu wa nchi.

“Tunatoka wito kwa wakuu wa nchi kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa ahadi na maazimio waliyoyaweka baada ya mkutano wao,” amesema.

Katika tamko hilo la pamoja, Walusala amevitaka vikundi vya waasi kukoma mara moja kuendelea na vita, kwa kuwa tayari watu wengi wameyakimbia makazi yao, huku wengine wakiuawa na kujeruhiwa.

“M23 wasimame mara moja kuendelea na vita kwa sababu watu wengi wameacha makazi, baadhi wameumia na wapo waliofariki,” amesema.

Iwapo mgogoro hautashughulikiwa kwa hatua za dharura, amesema kuna hatari ukaendelea kuwa hatari zaidi na hatimaye kusambaa nchi zote za Ukanda za Maziwa Makuu.

“Pia, tunavitaka vikosi vya kigeni vilivyoingia DRC bila kualikwa viondolewe, pia waathirika wa machafuko wapatiwe haki za kufidiwa,” amesema.

Amesema kuna umuhimu wa kanda yote kuwa na mtazamo wa pamoja ili kuwa na muitikio sawa katika kukabili matatizo ya kiusalama yanayoikabili DRC na ukanda kwa ujumla.

Related Posts