Maniche aingiwa ubaridi, City yajibu mapigo

Wakati mashabiki wa Mtibwa Sugar wakianza hesabu za vidole kwa chama lao kurejea tena Ligi Kuu, kocha wa timu hiyo Awadh Juma ‘Maniche’ amesema bado wana kazi kubwa ya kufikia malengo hayo, huku akieleza wanacheza kwa hofu ili kutotibua mipango.

Kauli ya kocha huyo inajiri baada ya kikosi hicho kilichoshuka daraja msimu uliopita kutoka suluhu na Mbeya City, katika mchezo wa Ligi ya Championship uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini Mbeya, huku ikionyesha mwelekeo mzuri hadi sasa.

Katika mchezo wa leo, timu zote zilizonyesha soka safi na la ushindani kwa kila upande ukihitaji ushindi ambapo wenyeji walishindwa kutakata baada ya kukosa penalti kupitia kwa Eliud Ambokile kunako dakika ya 54 ya mchezo huo wa kusisimua.

“Sisi benchi la ufundi bado hatujaanza hesabu kwa kuwa haijajulikana nani wa kupanda ila tunataka kati ya zile timu mbili za juu Mtibwa Sugar tuwemo, tunacheza kwa hofu kubwa sana ili tu kulinda matokeo yetu na kutimiza malengo tuliyoweka.”

Kwa upande wa kocha wa makipa wa Mbeya City, Juma Bukoli amesema mechi dhidi ya Mtibwa ilikuwa muhimu sana kwao kuchukua pointi tatu, lakini hali ya uwanja na kukosa umakini kwa nyota wao imewapa pointi moja na wataendelea kupambana zaidi.

“Makosa yameonekana na benchi la ufundi tutakaa kuyafanyia kazi haswa eno la ushambuliaji ukizingatia penati tuliyokosa imetupa ugumu, tulijiandaa kwa ushindi, ila kupata pointi moja ni jambo nzuri kwa sababu hatujapoteza,” amesema Bukoli.

Matokeo hayo yanaifanya Mtibwa kuendelea kusalia kileleni mwa msimamo na pointi zake 45, baada ya kushinda 14, sare tatu na kupoteza mmoja, huku Mbeya City ikisalia ya tatu na pointi 36, kufuatia kushinda 10, sare sita na kupoteza miwili.

Related Posts