MBEYA, JESHI LA POLISI LINAWASHIKILIA WAWILI KWA TUHUMA ZA KUKUTWA NA SILAA

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili Nerbat Mwasile Bwiga [33] Mkazi wa Ifumbo na Isaya Julias Zumba [38] Mkazi wa Airport Songwe kwa tuhuma ya kupatikana na silaha bunduki moja aina ya Shortgun Pump Action bila kuwa na kibali cha umiliki wa silaha hiyo.
Awali mnamo Aprili 29, 2023 majira ya usiku huko maeneo ya Nzovwe Jijini Mbeya, watuhumiwa walivunja Jengo la Black Microfinance Bank na kuiba silaha hiyo. Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya ufuatiliaji na mnamo Mei 11, 2024 huko Kijiji cha Itete kilichopo Kata ya Isuto, mkoani Mbeya lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Nerbat Mwasile Bwiga [33] akiwa na silaha hiyo.
Aidha, mtuhumiwa alikiri kuitumia silaha hiyo katika matukio mbalimbali ya uhalifu kwa kushirikiana na mtuhumiwa mwenzake aitwaye Isaya Julias Zumba [38]. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na mahojiano ili kupata mtandao mzima wa watu wanaojihusisha na matukio hayo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa jamii kutafuta kazi halali ya kufanya na kuachana na uhalifu kwani hauna nafasi ndani ya Mkoa wa Mbeya. Aidha, linatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu na wahalifu ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Related Posts