amewataka vijana wilayani Tarime Mkoa wa Mara kuacha kutumika kisiasa kwa lengo la kusababisha fujo na machafuko ndani ya wilaya hiyo.
Akizindua ofisi ya CCM Kata ya Nyakonga wilayani Tarime leo Jumapili Februari 9, 2025, Wasira amesema baadhi ya vijana wilayani humo wanatumika vibaya kwaajili ya kufanikisha malengo ya baadhi ya vyama vya siasa na wanasiasa, lakini wao hawanufaiki na chochote.
Amesema kwa muda mrefu vijana hao wamekuwa wakitumiwa kama chambo cha kuvuruga amani na baadhi ya wanasiasa, hasa nyakati za chaguzi na maandamano.
“Chadema wakitaka kufanya fujo mahari wanakuja kuchukua vijana kutoka Tarime, wanafanya vijana wa Tarime wanakuwa majeshi ya kukodisha,” amedai Wasira.
Nakuongeza kuwa, “Vijana kataeni kutumika vibaya, ni vema mkatumia nguvu zenu kwa manufaa ya jamii kiuchumi na hata kama ni siasa ziwe siasa zenye tija, hakuna sababu ya kujihusisha na siasa zenye kuleta vurugu na kurudisha nyuma maendeleo ya wilaya na mkoa wetu,” amesema.
Wasira amesema wilaya ya Tarime ni wilaya pekee ndani ya mkoa huo yenye rasilimali na fursa nyingi ambazo zinaweza kutumika vizuri kwa kufaidisha jamii katika nyanja ya uchumi na kwamba ni vema vijana wakatumia fursa hizo kujiendeleza kiuchumi na kuacha kutumika vibaya.
Hata hivyo, Mwananchi imezungumza kwa simu na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche ambaye amemtaka Wasira kutafakari kauli zake na kupunguza ukali wa maneno.
“Kwa huo muda tu mfupi Wasira anaongea vitu ambavyo havifanani na msingi wa umri wake, hazifanani na msingi wa siasa ambazo tungejifunza kama vijana na vimekuwa very viral (vimevuma) na kwa kweli vinanishanganza,” amesema Heche.
Amesema kwa kuwa Wasira ni Msabato kama alivyotangaza hadharani, afuate somo la saba la uadilifu na haki kwa kuwa ndiyo msingi wa serikali ya Mungu na siyo mizania ya uongo.
“Hata leo alikuwa kwenye minada, aliposimama pale ni Chadema…ni chademaaa ametoka huko kwenye mnada ameenda huko Mugumu..shida ninayoiona mzee wetu apunguze propaganda chonganishi.
“Kauli ya Makamu Mwenye kiti wa CCM taifa isipofanyiwa digestion vizuri inaweza kuleta mpasuko mkubwa sana. Huyu mzee anasema watu waje kwenye maridhiano…huyu mzee anatukana sasa unapotukana unapunguza tatizo au unaongeza gesi,” amehoji Heche.
Amesema ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama hicho ngazi ya mkoa na kwamba kwa uelewa alio nao nafasi Wasira alitakiwa kutumia muda mwingi kuleta mazingira rafiki ya kisasa nchini pamoja na kushauri vyama hivyo.
“Mercenary ni mtu anayetoka eneo jingine kwenda kufanya kitu kingine ambacho hakina maslahi. Sisi Chadema tuna katiba ya chama na vijana wote ambao wapo kwenye nchi hii, wana haki ya msingi kujiunga na vyama vya visiasa, Wasira anasema tunakodiwa kwenda kufanya fujo kwa mfano sisi tumefanya fujo wapi na lini,” amehoji mwenyekiti huyo.
Amesema kwa miaka takribani mitano hawajashiriki uchaguzi wowote huku akihoji vijana wa Tarime anaowasema Wasira walienda kufanya fujo hizo wapi.
Mkazi wa Tarime, Mariam Edward amesema kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu, vijana wanapaswa kuwa mabalozi wa amani na kuwakataa wanasiasa wanaotaka kuwatumia kuleta fujo na mivurugano katika jamii.
Katika hatua nyingine, Wasira akiwa wilayani Serengeti ameiagiza Wizara ya Mali Asili na Utalii kuangalia njia ya kudumu kutatua mgogoro baina ya wananchi na wanyama waharibifu wa mazao.
Amesema kwa muda mrefu kumekuwepo na changamoto hiyo ya wanyama kuvamia mashamba na kuharibu mazao ya baadhi ya wakazi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Taifa ya Serengeti jambo ambalo limekuwa likiwaathiri wananchi hao ikiwa ni pamoja na kuwasababishia njaa.