FIA yaipa Tanzania raundi ya tano ya ARC

CHAMA cha mchezo wa mbio za magari duniani, FIA kimetoa kalenda mpya ya mbio za magari ubingwa wa Afrika na Tanzania itaandaa raundi ya tano na si ya nne kama ilivyotangazwa awali.

Kalenda hii mpya imesambazwa kwa wadau wa mchezo wa mbio za magari nchini na Chama kinachosimamia mchezo huu, AAT(Automobile Association of Tanzania).

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya mbio za magari nchini, Satinder Birdi, mabadiliko ya kalenda yanazihusu zaidi nchi za Rwanda, Burundi na Tanzania na si Kenya na Uganda ambazo tarehe za mashindano yao hazijabadilika.

Kalenda ya awali iliyotolewa na FIA  ilionyesha mbio za Mountain Gorilla za Rwanda ndizo zingefunga msimu wa mwaka 2025, mwezi Novemba baada ya Tanzania kukamilisha raundi yake mwezi Septemba mwaka huu.

Kalenda mpya iliyotolewa na FIA inaonyesha msimu wa mbio za magari ubingwa wa Afrika unaanza rasmi Machi 20 hadi 23 kwa raundi ya kwanza ya ARC itakayochezwa Kenya na kujulikana kama Equator Rally.

Mbio za Equator pia zitaenda sambamba na mbio za magari ubingwa wa dunia, World Rally Championship (WRC).

Mbio za Uganda maarufu kama Pearl of Africa Rally zitafuata Mei 9 hadi 11 kabla ya kuhamia Rwanda ambako mbio zitachezwa Julai 4 hadi 6 kwa raundi ya tatu.

Burundi itaandaa raundi ya nne Agosti 15 hadi 17, kabla ya Tanzania kufunga msimu kwa mchezo utakaochezwa mkoani Morogoro Septemba 19 hadi 21.

Tangu kuasisiwa kwake mwaka 1953, kama mbio maalum za kumbukumbu ya kutawazwa Malkia Elizabeth wa Uingereza, mbio za magari, zikijulinana kama East African Safari Rally, zimekuwa zikichezwa sana katika ukanda wa Afrika ya Mashariki, zikitembelea maeneo muhimu ya kiutalii na kihistioria katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania kabla ya kubadilishwa na kujulikana kama World Rally Championship(WRC) kutokana na kukosekana kwa udhamini maridhawa Afrika ya Mashariki.

Morogoro ambayo itaandaa raundi ya tatu ya ubingwa wa taifa Agosti 9 na 10, pia itakuwa mwenyeji wa raundi ya tano ya ARC Septemba mwaka huu.

Related Posts