Majaji wa Mahakama Kuu nchini Marekani jana, Jumamosi, walipitisha azimio la kumzuia Mkuu wa Idara ya Ufanisi wa Taasisi za Serikali (DOGE), Elon Musk, kuingia kwenye mfumo wa taarifa au kuzifikia nyaraka zote za hazina kwa maelezo kuwa ni kinyume cha sheria.
Inaelezwa kuwa Musk, aliyeteuliwa na Rais Donald Trump kwa lengo la kufuatilia ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji wa serikali, alikuwa akitaka kuingia kwenye taarifa za mfumo mkuu wa malipo ya serikali unaosimamiwa na Department of Treasury (Hazina), kwa lengo la kukagua malipo yote yanayofanywa na serikali.
Mfumo huo unahifadhi taarifa zote muhimu kama malipo ya kodi, malipo ya mifuko ya hifadhi za jamii, mafao ya wastaafu, na malipo mengine ya aina hiyo, ambapo matrilioni ya dola za Kimarekani hulipwa kila mwaka.

Uamuzi wa majaji hao umeeleza kwamba taarifa hizo ni nyeti na Musk hana ruhusa ya kisheria ya kuzifikia, hata kwa maagizo ya rais, mpaka shauri la msingi litakaposomwa na kutolewa uamuzi na mahakama, Februari 14, 2025.
Mahakama hiyo pia imeamuru Musk ateketeze nyaraka zote ambazo ameshazipata kabla ya uamuzi wa jana, mpaka mahakama itakapotoa uamuzi wa mwisho kuhusu suala hilo.