Elon Musk, Malema warushiana maneno mtandaoni, madai ya ubaguzi

Dar es Salaam. Mmiliki wa mtandao wa X na mfanyakazi katika kitengo cha ufanisi wa Serikali ya Marekani, Elon Musk, amerushiana maneno na Kiongozi Mkuu wa chama cha EFF cha Afrika Kusini, Julius Malema kwa kile alichomshutumu kuwa ni mbaguzi na mleta machafuko.

Mvutano huo uliotokea jana, Februari 9, 2025, katika mtandao wa X, ulitokana na video ya Malema ya mwaka 2018 iliyochapishwa tena jana, ambapo Malema alisema, “Tutakata koo la watu weupe,” akimaanisha kumuondoa aliyekuwa meya (mzungu) wa Nelson Mandela Bay, Athol Trollip.

Musk alirejelea kauli hiyo na kumtaja Malema kama mhalifu wa kimataifa, akitoa wito wa kuwekewa vikwazo vya haraka dhidi yake.

“Vikwazo vya mara moja kwa Malema na atangazwe kuwa mhalifu wa kimataifa,” aliandika Musk akiijibu video hiyo ya Malema iliyopostiwa na Mario Nawfal, ambaye ni miongoni mwa watumiaji maarufu wa mtandao wa X.

Baada ya Musk kuandika hivyo, Malema alimjibu kuwa hataacha kupigania haki za watu weusi na kutaka usawa, huku akimtuhumu Musk kunufaika na unyonyaji unaofanywa na watu weupe.

“Kwa kweli, nadhani umepoteza kabisa ubongo wako wa kushoto: shujaa wa kawaida aliyeharibiwa na mnufaika wa moja kwa moja wa weupe wa ubaguzi wa rangi.

“Najua watu weusi wanafanana na wewe, mbaguzi wa kawaida. Angalia kwa karibu, na utagundua hao ni watu wawili tofauti. Marekani inatudhihirishia ujinga wake. Sijali kuhusu vikwazo vyako; sitaacha kamwe kupigania watu weusi wawe sawa na weupe, na hilo likinifanya kuwa mhalifu wa kimataifa, ninajivunia kuwa mmoja,”* aliandika Malema.

Mnyukano huo kati ya Malema na Musk uliibua mjadala katika mtandao wa X, huku maoni mchanganyiko yakitolewa.

Related Posts