BAADA ya kukwama kutua KMC iliyokuwa ikimpigia hesabu dirisha dogo, mshambuliaji matata wa Tabora United, Offen Chikola imedaiwa sasa ameingia anga za vigogo wanaomtaka kwa ajili ya msimu ujao wa 2025-2026.
Taarifa kutoka kwa watu wa karibu wa mchezaji huyo, zinasema mabosi wa Simba na Yanga wame-anza kupigana vikumbo, kuulizia mkataba wa Chikola anayemiliki mabao manne hadi sasa ikiwa ni msimu wake wa kwanza akiwa na kikosi hicho alichojiunga nacho akitokea Geita Gold iliyoshuka daraja.
Inaelezwa, Yanga ni klabu ya kwanza kutaka huduma kwa mchezaji huyo na kuzungumza na meneji-menti yake, lakini wakajulishwa kwa sasa bado ana mkataba na Tabora, hivyo watulie.
Hata hivyo, Simba nao inadaiwa wameufuta uongozi wa mchezaji huyo ili kuulizia mkataba na kama wanaweza kumpata mwishoni mwa msimu huu kwa ajili ya msimu ujao, ikieleza mkataba wake unamalizika Mei mwaka huu.
Chanzo kutoka Simba kinasema endapo dili lake likitiki atakwenda kuongeza idadi ya mabao mbele ya Kibu Denis na Elie Mpanzu na wanaamini uzoefu wa mastaa hao utamjenga zaidi, kwani hadi sasa wawili hao waliopo Msimbazi hawajafunga bao lolote tofauti na Chikola mwenye manne.
“Chikola ni mzuri kwenye kufunga, uzoefu wa Kibu na Mpanzu utakwenda kumjenga na atakuwa bora zaidi, mazungumzo yanaendelea ila bado hayajafikia mwisho,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Tunajua Yanga iliwahi kumhitaji, lakini kama haijamsainisha timu yoyote inaweza ikapata huduma yake, ndiyo maana tunazingatia utaratibu kwa kuangalia mkataba wake unasemaje.”
Ukiachana na Simba na Yanga timu nyingine inayowania saini yake ni JKT Tanzania na katika nafasi yake kuna wachezaji kama Hassan Dilunga na Hassan Kapalata ambaye muda mwingine anatokea pem-beni, ingawa nafasi yake ni kiungo.
Alipotafutwa Chikola kuhusu taarifa hizo alisema; “Mimi bado ni mchezaji wa Tabora United, siwezi kuanza kuzungumzia habari hizo, kama kuna timu zinazonihitaji naamini zinajua utaratibu zitapaswa kwen-da kwa uongozi wangu,” alisema Chikola aliyewahi kukipiga Ndanda enzi ikiwa Ligi Kuu kisha kutua Geita aliyoitumikia misimu mitatu kabla ya msimu huu kutua Tabora iliyopo msimu wa pili Bara.
Jina la Chikola lilikuwa gumzo mapema msimu huu baada ya kufunga mabao mawili kati ya matatu yaliyoiua Yanga nyumbani kwa 3-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara na kuwa chanzo cha kutimuliwa kwa kocha Miguel Gamondi. Kabla ya mechi hiyo Yanga ilitoka pia kupoteza 1-0 mbele ya Azam FC.