NYOTA wa Kitanzania, Malaika Meena amesema ana furaha kubwa kujiunga na Bristol City inayoshiriki Ligi ya Wanawake ya Championship ya England, huku akitaja malengo yake ni kuipandisha timu ligi kuu.
Wikiendi iliyopita Mtanzania, Malaika Meena alisaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo wenye kipengele cha kuongezewa ikiwa atafanya vizuri.
“Nina furaha kubwa kusaini na Bristol City, hasa kwa sababu ya malengo makubwa kwa klabu hii ni kupambana kwa ajili ya kupanda daraja,” alisema Malaika baada ya kusaini mkataba.
Malaika anakuwa mchezaji wa pili kucheza England baada ya Aisha Masaka anayekipiga Brighton Hove $ Albion inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini humo.
Timu hiyo iko nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo unaoshirikisha timu 11 ikikusanya pointi 23, tofauti ya alama tatu na kinara Birmingham yenye 26.
Chama hilo liko kwenye nafasi nzuri ya kupanda daraja msimu ujao, hivyo usajili wa kiungo huyo Mtanzania, timu hiyo inaamini ataisaidia kuipandisha.
Nyota huyo aliyeitwa kwenye kikosi cha Twiga Stars kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcon 2026), amewahi kupita timu za vijana za Chelsea na Arsenal kabla ya kutimkia Wake Forest ya Marekani alikosaini mkataba wa miaka mitatu na nusu.