Wanajeshi 75 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanatarajiwa kufikishwa kizimbani leo wakikabiliwa na mashtaka ya kukimbia mapigano, pamoja na kufanya vurugu dhidi ya raia, ikiwemo mauaji na uporaji. Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi iliyotolewa Jumapili, wanajeshi hao walikamatwa baada ya kushikiliwa kwa mji wa Nyabibwe na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.
Umoja wa Mataifa umeripoti ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na unyongaji, ubakaji wa magenge, na utumwa wa kingono, kufuatia msako mkali wa waasi wa M23 mwishoni mwa Januari ambao ulisababisha kutekwa kwa mji wa Goma. Ripoti hiyo inawalaumu waasi wa M23, askari wa serikali, na wanamgambo wanaounga mkono serikali kwa uhalifu huo.
Hata hivyo, Kongo haijatoa tamko rasmi kuhusu tuhuma hizo lakini imeutaka Umoja wa Mataifa kuchunguza ukiukwaji wa haki unaodaiwa kufanywa na waasi wa M23 na Rwanda. Rwanda imekanusha kuunga mkono M23, huku waasi hao wakikataa kutoa maoni yao kuhusu tuhuma hizo.
Licha ya tangazo la kusitisha mapigano kwa upande mmoja, waasi wa M23 wameendelea kusonga mbele kuelekea Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini. Mashirika ya kiraia yameripoti kuwa wanajeshi waliotoroka wamewaua watu 10 katika mji wa Kavumu, wakiwemo saba waliokuwa kwenye baa siku ya Ijumaa jioni.
Msemaji wa jeshi la mkoa huo, Nestor Mavudisa, amesema askari hao watachukuliwa hatua kali za kisheria na kuwataka wananchi kuwa watulivu.
Kwa sasa, hali imetulia kiasi, ingawa mapigano bado yanaripotiwa katika mbuga ya kitaifa iliyoko kilomita 30 kutoka Bukavu, pamoja na milio ya risasi ya hapa na pale katika eneo hilo.
Katika juhudi za kumaliza mgogoro huo, viongozi wa Afrika walikutana mwishoni mwa juma na kuzitaka pande zote mbili kufanya mazungumzo ya moja kwa moja. Serikali ya Kongo imesema imezingatia maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano huo.