BAADA ya kuikalia kooni Simba Queens hadi dakika za jioni ikichapwa bao 1-0, Ceasiaa Queens imesema imeanza mipango ya kuzisaka pointi sita mbele ya Get Program na Bunda Queens.
Wikiendi iliyopita timu hiyo ilikuwa mgeni wa Simba Queens Uwanja wa KMC Complex ikichapwa bao 1-0 dakika za jioni na Jentrix Shikangwa na kuifanya mnyama aendelee kusalia kileleni.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa timu hiyo, Ezekiel Chobanka alisema wameanza mipango ya kupambania pointi sita dhidi ya Get Program na Bunda ili kujihakikishia timu hiyo inakaa nafasi ya nne.
Chobanka alisema kwa sasa anatengeneza timu ingawa kuna mabadiliko ya muunganiko wa timu tofauti na hapo awali alipofika.
Ikumbukwe kocha huyo alikuwa Alliance Girls kabla ya kuhamia Ceasiaa dirisha dogo na tayari amesimamia mechi nne akishinda mbili na kupoteza mbili.
“Kama ilivyo msimu uliopita tunatamani kumaliza nafasi ya nne lakini kabla ya hapo napaswa kushinda mechi mbili za viporo ambazo kama tukipata pointi zote basi nina uhakika wa kumaliza katika nafasi hizo,” alisema Chobanka.
Kuhusu maingizo mapya dirisha dogo kama yamebadilisha kitu kwenye kikosi chake, anajibu.
“Tumesajili wachezaji wa kigeni na wengine wa ndani hadi sasa siwezi kusema moja kwa moja kwa sababu wamecheza mechi chache lakini wamejitahidi kuendana na kasi ya ligi, mfano kuna straika hata mazoezi hakufanya vizuri na timu lakini anafanya vizuri.”
Timu hiyo iko nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi raundi ya 12 ikiwa imecheza michezo 10 ikikusanya pointi 10 ushindi tatu, sare moja na kupoteza sita.