Dar es Salaam. Baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Mbeya kutupilia mbali moja kati ya kesi mbili zilizofunguliwa mahakamani hapo na wananchi kutoka vijiji 23 vikipinga kusudio la Serikali kutaka kuvifuta, sasa wananchi hao wanakwenda Mahakama ya Rufani kupambana kurejesha kesi hiyo ili wapate kusikilizwa.
Hiyo ni moja kati ya kesi tatu, zilizofunguliwa na wanavijiji hao wakipinga kusudio la Serikali kutaka kuwahamisha katika makazi yao kwa madai ya kuvamia eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Kesi hiyo ya ardhi namba15/2023 ilikuwa imefunguliwa na Ezekia Kimanga na Modestus Kilufi wakiwawakilisha wenzao wengine 859 dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Vijiji hivyo vilivyo katika mgogoro huo ni Mahango, Mkunywa , Ikeha, Nyangadete, Magigiwe, Vikaye, Igunda, Ivalanji, Ikanutwa, Nyeregete, Mwanavala, Ibumila, Songwe, Warumba, Ukwavila, Kapunga, Iyala, Luhanga, Madundasi, Msanga, Simike, Kilambo na Udindilwa.
Hata hivyo Mahakama hiyo imeitupilia mbali kesi hiyo kabla ya kusikilizwa madai ya msingi, kufuatia pingamizi la awali lililoibuliwa na Serikali (wadaiwa).
Uamuzi huo umetolewa Januari 31, 2025 na Jaji Mussa Pomo baada ya kukubaliana na hoja ya pingamizi la Serikali kuwa hati ya madai haina maelezo ya kutosha kubainisha eneo la ardhi ya kila mdai inayobishaniwa, kama sheria hiyo inavyotaka.
Wakizingumzia uamuzi huo kwa nyakati tofauti, leo Jumatatu, Februari 10, 2025, mawakili wa wanavijiji hao Edson Mbogoro na Jebra Kambole wamesema hawajaridhishwa na uamuzi huo na kwamba wanakata rufaa Mahakama ya Rufani kuupinga.
“Kwa hiyo tuko katika maandalizi na tunatarajia kuwa kuwa wiki ijayo tutawasilisha notisi (taarifa) ya kusudio la kukata rufaa na kisha tutasubiri kupata mwenendo wa shauri kwa ajili ya kuwasilisha sababu za rufaa yetu,” amesema Wakili Mbogoro.
Wakili Kambole amesema kuwa uamuzi huo haukubaliki kwa kuwa katika mazingira ya kesi hiyo ilichokisema Mahakama katika uamuzi wake ni vigumu kutekelezeka.
“Hii ni kesi ya uwakilishi, na kulingana na idadi ya wadaawa ni jambo lisilowezekana kuweka maelezo ya ardhi anayoimiliki kila madai katika hati moja,” amesema Wakili Kambole na kuhoji:
“Hapa Kuna wadai zaidi ya 800, hivi ukiweka maelezo ya eneo la kila mdai kama Mahakama ilivyosema hiyo hati itakuwa ya namna gani?”
Hata hivyo Wakili Kambole amesema kila mdai aliwasilisha biambatisho kuonesha eneo analolimiliki kwamba wangeweza kuyathibitisha hayo wakati wa usikilizwaji wa kesi.
“Hivyo tunakwenda Mahakama ya Rufani ili itoe msimamo wake na tunaamini kuwa Mahakama ya Rufani itatolea ufafanuzi na kitofautisha kati ya kesi ya uwakilishi na kesi za kawaida,” amesema Wakili Kambole.
Mbali na kesi hiyo wakili Mbogoro amesema kuwa bado kuna kesi nyingine kama hiyo mahakamani hapo ambayo imepangwa kusikilizwa Februari 18 na Jaji Victoria Nongwa na nyingine waliyoifungua Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki ambayo wanadubiri kupangiwa ya tarehe ya usikilizwaji.
Taarifa ya kusudio la kuwahamisha wanavijiji hao ilitolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Oktoba 25, 2022, katika mkutano na wanavijiji hao.
Kufuatia taarifa hiyo wanavijiji hao walifungua kesi hizo tatu baada ya kukamilisha taratibu za kisheria za kuishtaki Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa notisi ya kusudio hilo ya siku 90, mbili Mahakama Kuu Mbeya na nyingine moja Mahakama ya Afrika Mashariki.
Katika kesi hiyo waliiomba mahakama hiyo itamke kuwa wao ni wakazi halali wa vijiji hivyo 23, wamiliki halali wa ardhi hiyo yenye mgogoro na kwamba uhamishwaji uliokuwa unakusudiwa na mchakato wa uthamini uliokuwa unaendelea ulikuwa ni batili.
Pia waliiomba mahakama hiyo iamuru walipwe fidia ya hasara halisi ya Sh2 bilioni, fidia ya madhara ya jumla Sh950 bilioni na itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya wadaiwa.
Katika mbadala wake waliomba kuea ikiiwa itabidi wahamishwe basi wadaiwa wafuate sheria ya Ardhi kuhusu kuhamishwa na kufidiwa.
Wadaiwa waliibua pingamizi la kisheria wakiiomba Mahakama iitupilie mbali kesi hiyo kabla ya kuisikiliza wakidai kuwa haikuwa na ustahilifu na ni batili kisheria kwa kukiuka Amri ya VII Kanuni ya 3 ya Sheria ya Mwenendo wa Madai (CPC), marekebisho ya mwaka 2019.
Pingamizi hilo lilisikilizwa kwa njia ya maandishi na wadaiwa waliwakilishwa na Wakili wa Serikali Michael Fyumagwa.
Wakili Fyumagwa alidai kesi hiyo inahusisha mali isiyohamishika, hivyo hati ya madai ilipaswa kuwa na maelezo ya kutosha kubainisha eneo la ardhi inayobishaniwa, kama sheria hiyo inavyotaka, kwamba kila mdai kubainisha, ukubwa, mipaka na majina ya wamiliki anaopakana nao.
Akijibu hoja hiyo wakili Mbogoro alidai kila kesi inapaswa kuamuriwa kwa upekee wa maelezo na mazingira yake.
Alidai kuwa kesi hiyo ni kesi ya uwakilishi iliyofunguliwa chini ya Amri ya I Kanuni ya 8 ya CPC, ikihusisha eneo kubwa ambalo huathiri wadaawa wengi wenye haki na maslahi yanayofanana.
Hivyo alidai kuwa maelezo ya kiujumla yaliyoko kwenye hati ya madai katika aya mbalimbali (akizitaja), yanakidhi matakwa ya Sheria kwani yanatosha kubainisha eneo lenye mgogoro kwa kuzingatia asili ya kesi yenyewe.
Aliongeza kwamba katika kutimiza matakwa ya kesi ya uwakilishi
wadai wameambatanisha maelezo muhimu kubainisha eneo lenye mgogoro, huku akiirejesha mahakama katika kesi mbalimbali zilizokwishakuamuriwa na mahakama hiyo na Mahakama ya Rufani
Jaji Pomo katika uamuzi wake amesema kwa aina hiyo ya kesi, Kanuni ya 3 Amri ya VII ya CPC inaweka sharti la lazima hati ya madai kuwa na maelezo yanayotosheleza kubainisha mali inayobishaniwa.
Amesema baada ya kusoma aya zote 21 zinazoiunda hati ya madai ameridhika kuwa hazitoi maelezo ya kutosheleza kubainisha ardhi ya kila mdaiwa yenye mgogoro, kinyume na yale wakili Mbogoro alivyoeleza wakili Mbogoro.
“Hivyo kwa ukiukwaji huo (wa Sheria) kama ulivyoshambuliwa na wadaiwa, kesi hii haina ustshilifu mbele ya Mahakama hii, kwa kutokuwa na maelezo ya madai yanayotosheleza kubainisha, jambo ambalo no kinyume na Kanuni ya 3 Amri ya VII ya CPC,” amesema Jaji Pomo na kuhitimisha:
“Kwa kusema hayo, naona kuwa pingamizi lililoibuliwa kina mashiko na ninakikubali. Kwa hiyo kesi hii haina ustahilifu na inatupiliwa mbali,” amedai.