‘ACT Wazalendo kuunda Serikali kwa falsafa jumuishi’

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema chama hicho kinaamini kuunda Serikali kwa kutumia falsafa jumuishi ambayo haitabagua vijana Wazanzibari kutokana na itikadi na imani za vyama vyao tofauti vya siasa.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameyasema hayo viwanja vya Stela Daraja bovu Welezo Wilaya ya Magharib A Unguja jana Jumapili Februari 9, 2025 alipohutubia wananchi, wafuasi na wanachama wa chama hicho.

Othman amesema vijana hawapaswi kufanya makosa ya kutokiunga mkono chama hicho kwani ndio chama pekee kinakusudia kuinyoosha nchi na kuwakabidhi vijana ili washindane katika kuipeleka mbele nchi yao kwa kuwa ubaguzi hauwezi kusaidia katika kujenga maendeleo ya taifa.

“Ni muhimu kujenga utawala mwema utakaoheshimu maamuzi ya wananchi kwa kuwa ufalme wa nchi ni wananchi wenyewe na kwamba ndio wenye maamuzi juu ya namna wanavyotaka nchi yao iendeshwe,” amesema.

Amesema Zanzibar inazo rasilimali nyingi za kiuchumi na pia imebahatika kuwepo katika eneo muhimu na zuri la kijiografia katika kuendesha shughuli za kibiashara na kwamba inaweza kuleta mafanikio na kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo kwa muda mfupi iwapo itasimamiwa vyema.

Wananchi, wafuasi na wanachama Cha ACT Wazalendo wakiwa kwenye mkutano wa hadhara Daraja Bovu wakati Mwenyekiti wa Chama hicho Tafa, Othman Masoud akiwahutubia

Kwa muktadha huo, amewataka Wazanzibari katika uchaguzi mkuu ujao Oktoba 2025 kutofanya makosa na kuhakikisha wanakiunga mkono chama ca ACT ili kuleta mageuzi ya kweli kiuchumi na kisiasa na kuifanya Zanzibar kuwa na mamlaka yake katika kusimamia nyenzo zake za kiuchumi.

Amesema kwamba kinachohitajika ni kuwepo uchaguzi huru na haki wenye ushindani wa Kidemokrasia na kuwataka wananchi wa Zanzibar kukiunga mkono chama hicho ambacho kinakusudia kutetea haki za Zanzibar na kuchagiza kasi ya maendeleo ya wananchi.

Kwa upande wako, mwakilishi wa Ngome ya wanawake kutoka Mkoa wa Magharib A kichama, Asha Mussa amawataka vijana kuhakikisha wanakwenda kujiandikisha na kwamba wazazi wanawajibu wa kuwashajiisha watoto wao kufanya hivyo ili kuleta mageuzi ya kweli muda wa uchaguzi utakapowadia.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho, Nassor Ahmed Mazrui amewataka vijana kutambua kwamba wanawajibu na jukumu kubwa katika kukiunga mkono chama hicho ili kufanikiwa kuleta mageuzi muhimu ya kimaendeleo yanayohitajika Zanzibar.

Mazrui ambaye pia ni Waziri wa Afya Zanzibar amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika awamu hii ya pili na mwisho ya uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura, kazi hiyo ambayo ilianza Februari mosi inaendelea katika visiwa hivyo.

Related Posts