KOCHA Fadlu Davids kesho ana kazi ya kuiongoza Simba kurekebisha ilipokosea mechi iliyopita itakapoikaribisha Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar kuanzia saa 10 jioni.
Fadlu ambaye anapambana kuirudisha Simba kileleni mwa msimamo wa ligi, alishuhudia mechi iliyopita wakiambulia sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Fountain Gate – matokeo yaliyotibua rekodi yake ugenini kwani alikuwa ameshinda nane kabla ya kusimamishwa.
Simba inakutana na Tanzania Prisons, timu ambayo duru la pili imeanza kwa ushindi wa mechi mbili mfululizo dhidi ya Pamba Jiji (1-0) na Mashujaa (2-1).
Tanzania Prisons iliyopoteza mchezo wa duru la kwanza dhidi ya Simba kwa bao 1-0 nyumbani, hivi sasa inafundishwa na Kocha Amani Josiah aliyechukua mikoba ya Mbwana Makata aliyesitishiwa mkataba Desemba 28, 2024.
Katika mchezo wa kesho, Tanzania Prisons itataka kufanya mambo mawili – kwanza kuendeleza rekodi ya ushindi duru la pili baada ya kutofanya vizuri lile la kwanza ilipocheza mechi 15 na kushinda mbili, sare tano na kupoteza nane ikikusanya pointi 11 ikiwa katika mstari wa hatari kushuka daraja.

Wakati Prisons ikiwaza hivyo, Simba inataka ushindi ili kuendelea kuwa na matokeo mazuri uwanja wa nyumbani baada ya kushuhudiwa msimu huu kupoteza moja na sare moja kwenye mechi nane za nyumbani.
Rekodi zinaonyesha timu hizo mechi 10 za mwisho Simba imeshinda tano, Prisons ikishinda tatu na sare mbili huku nyingi mabao yakiwa machache. Moja iliyochezwa Desemba 30, 2022, Simba ilishinda 7-1 huku zingine mabao matatu kushuka chini.
Vita ya namba mbili na tatu
Hii ni mechi inayozikutanisha timu zinazopambana kukaa sehemu nzuri zaidi. Simba iliyopo nafasi ya pili kutoka juu kwenye msimamo na pointi 44, inahitaji kufanya vizuri kurudi kileleni ambapo Yanga ndiyo imeshikilia nafasi hiyo.
Kwa upande wa Prisons inashika nafasi ya tatu kutoka chini, hivyo haipo salama sana ikihitaji kupanda juu.

Maafande hao wa Magereza wana pointi 17 baada ya mechi 17 wakiwa na wastani wa kupata pointi moja kila mechi jambo linaloashiria kuna changamoto wanahitaji kuifanyia kazi.
Kitendo cha kuanza duru la pili vizuri kinamfanya kocha Josiah kuamini wana nafasi ya kuendelea kupata matokeo hayo licha ya kukiri wanakutana na mpinzani aliye juu yao kwa uwezo, lakini kutokuwa na majeruhi wapya ni faida kwao.
“Jambo zuri ni kwamba hatuna majeruhi katika wachezaji tulioanza nao raundi ya pili. Kikosi kilichomaliza mechi ya mwisho (dhidi ya Mashujaa) wote wapo vizuri na waliokosa leseni wamepata, hivyo inatoa mwelekeo mzuri kuelekea mechi hii.
“Ninachoweza kuwaambia wachezaji wangu timu kama Tanzania Prisons kufungwa na timu kubwa kama Simba, Yanga na Azam sio stori, hivyo siwapi presha, waende wakainjoi mechi sitaki kuwaambia lazima washinde kwani nitawapa presha, kama wana kitu cha ziada watakachofanya kupitia kujiamini kwao, nitafurahi.

“Hatuwezi kupambana na Simba asilimia 50 kwa 50 katika suala la kumiliki mpira, nitakuwa nadanganya. Lakini ninaamini tuna uwezo wa kuwa na nguvu kipindi ambacho Simba inamiliki mpira na sisi tunapokuwa na mpira tuna uwezo wa kufanya namna ya kuumiliki na sio kuupoteza,” alisema Josiah.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids anaamini wanakutana na timu ngumu yenye benchi jipya la ufundi tofauti na ilivyokuwa duru la kwanza hivyo wanapaswa kujipanga sawasawa.
Fadlu amebainisha kwamba wataendelea na mbinu za kushambulia sana huku malengo yakiwa ni kufunga mabao ya mapema.
“Tumejiandaa kwa mechi hii. Tanzania Prisons ni timu ngumu, kwa sasa wana kocha mpya mwenye mbinu tofauti.
“Ninakubali kwamba duru la pili mechi ni ngumu kila timu inacheza kutafuta kitu cha tofauti,” alisema.

“Sisi kila mechi huwa tunafanya uchambuzi ikiwa ni sehemu ya maandalizi yetu. Tutaendelea na mtindo wetu wa uchezaji kwa kutengeneza nafasi nyingi. Malengo yetu ni kujaribu kufunga mabao mapema kwani unapofanya hivyo unamfanya mpinzani kupoteza kujiamini lakini ikitokea muda mrefu matokeo ni 0-0 basi anaona kuna kitu anaweza kupata.”
Fadlu aliongeza kuwa Kibu Denis bado yupo kwenye uangalizi na mazoezi ya jana yalitumika kumuangalia zaidi kama anaweza kuwepo katika mchezo, huku akigusia ishu ya Ladack Chasambi akisema kama klabu wamechukua jukumu la kumlinda asitoke mchezoni akiamini bado ni kijana mdogo mwenye kipaji kikubwa.
“Chasambi ana kipaji ni miongoni mwa wachezaji wadogo wanaofanya vizuri, ninamuamini siwezi kumlaumu kwa matokeo yaliyopita. Kama klabu tunasimama naye ili kulinda kipaji chake ambacho si faida kwa Simba pekee, bali Tanzania kwa ujumla,” alisema Fadlu baada ya kuwepo kwa maneno mengi kuhusu Chasambi ambaye mechi iliyopita alijifunga na kuifanya Simba kupata sare nyumbani kwa Fountain Gate.
Wakati Simba na Tanzania Prisons zikipambana, muda huohuo saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, Mashujaa itaikaribisha Coastal Union.
Mashujaa iliyototoka kufungwa 2-1 na Prisons ina nafasi ya kujiuliza mbele ya Coastal Union ambayo imetoka kushinda nyumbani.
Duru la kwanza Mashujaa ilishinda ugenini 1-0, hivyo Coastal itataka kulipa kisasi wakati Mashujaa ikihitaji kurekebisha makosa.
Kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera Sugar itakuwa wenyeji wa Tabora United katika mchezo utakaoanza saa 1:00 usiku. Kagera Sugar duru la pili imeanza kwa kuchapwa 4-0 na Yanga, lakini ikaikazia Singida Black Stars na kutoka sare ya 2-2, kumbuka mechi zote hizo ilikuwa ugenini na sasa inarudi nyumbani.