Morogoro. Kamishna Jerenali wa Magereza Tanzania, Mzee Nyamka amewataka watumishi wa jeshi hilo kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia sheria na waache kujihusisha na matendo yanayolitia doa jeshi hilo, ikiwamo kuwapiga wafungwa ambao baadhi yao wameshapoteza maisha.
Akizungumza leo Jumapili Aprili 20, 2024 mjini Morogoro wakati akifunga mafunzo ya uongozi daraja la kwanza ngazi ya sajenti kwa askari magereza wa mkoa huo, Nyamka amesema siku za karibuni kumekuwapo malalamiko kutoka kwa wafungwa wanaodai wapo baadhi ya askari na maofisa magereza huwapiga na kuwasababishia majeraha makubwa, ulemavu wa kudumu na hata vifo wakiwa ndani ya magereza.
“Sasa sitokubali kuona ofisa wa Jeshi la Magereza ninaloliongoza au askari kusababisha umauti kwa mfungwa au mahabusu, sitoruhusu mfungwa kupata ulemavu ndani ya Jeshi la Magereza katika kipindi anachotumikia adhabu yake au kuumizwa, ikitokea askari akijihusisha na matendo hayo, atafukizwa kazi kisha kukabidhiwa kwenye vyombo vya sheria, ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake,” amesema Nyamka na kuongeza;
“Nimekuwa nikipiga kelele kama mwendawazimu, watu hawanisikii halafu wananipa taarifa za uongo, kwenye Gereza la Utete lililopo Rufiji mkoani Pwani, mfungwa amepigwa amefariki dunia, naambiwa alijaribu kutoroka amejikwaa kwenye kisiki ndio sababu ya kifo, hii haikubaliki maofisa wote mnapaswa kubadilika.”
Hata hivyo, amesema tayari amemuagiza Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) afanye uchunguzi maalumu kuhusiana na kifo cha mfungwa huyo.
“Nilimuagiza DCI apeleleze, watakaobainika wamesababisha kifo cha mfungwa yule wafikishwe mahakamani kwa mujibu wa sheria,” amesema Kamishna Nyamka.
Amesema Gereza la Karatu pia kuna mfungwa aliyepigwa na askari magereza akiwa ndani ya gereza akapatiwa rufaa ya kwenda kutibiwa Hospitali ya Mount Meru Arusha.
Amesema mfungwa huyo (bila kumtaja jina), alivyopelekwa hospitali alikuwa hawezi kupumua mpaka alipowekea mashine ya kumsaidia kupumua. “Huko nako nimeagiza uchunguzi wa kina ufanyike.”
Amesema kuanzia sasa, askari magereza wote wanaojihusisha matendo yanayokwenda kinyume na maadili ya Jeshi la Magereza, watachukuliwa hatua kali ili liwe fundisho kwa wengine.
Amesema askari wengi ni waongo na hawatimizi majukumu yao ipasavyo, huku akisema siku hizi akiwatuma maofisa magereza kufanya uchunguzi wa jambo fulani, humletea taarifa za uongo na ubabaishaji.
“Sasa uchunguzi wa magereza utafanyika, pia nitamuomba DCI anisaidie maana nataka kuondoa kirusi hiki ambacho kimeota ndani ya Jeshi la Magereza, hiyo ni kwa upande wa Karatu,” amesema.
Akizungumzia suala la Loliondo, Kamishna Nyamka amesema alipokuwa njiani akitokea Dar es Salaam juzi kuelekea shule ya Sekondari Bwawani, aliambiwa Morogoro, kuna mfungwa ametoroka na askari walisaidiwa kumkamata na askari Polisi wa Mirelani.
Amesema alitaarifiwa kuwa maofisa wa magereza baada ya kukabidhiwa yule mfungwa, wakaanza kumpiga mpaka akafariki dunia.
“Kuna timu pia inachunguza, nimeituma kwenda Loliondo na nimeipa siku tatu waniletee taarifa maana ushahidi upo, nahitaji tu kujiridhisha ujinga ambao askari wa jeshi letu wameufanya,” amesema kamishna huyo.
Amesema ikibainika askari hao wamehusika na mauaji ya mfungwa huyo, hatua ya kwanza itakuwa kuwafukuza kazi na baadaye utaratibu wa kuwafikisha mahakamani utafuata.
“Tutawashitaki kwa tuhuma za mauaji ikibainika, nimechoka sasa maana nimepiga sana kelele, viongozi wa magereza wote tumekaa nao kikao, lakini hakuna mabadiliko,” amesema.
Amesema askari magereza wote wanapaswa kujua kwamba hiki anachokisisitiza si masihara, atakayepuuza madhara yake atayaona.
Amesema huko Iringa gereza la Isopilo, nako anataarifa za wafungwa kupigwa mpaka wamepelekwa hospitali kutibiwa.
Amesema Jeshi linaingia gharama kubwa ya kuwatibu wafungwa majeraha kwa sababu ya askari wasiozingatia maadili yao ya kazi.
Mwananchi Digital ilizungumza na Jumanne Hamza, mfungwa aliyemaliza kifungo chake katika gereza la Isanga, mkooani Dodoma na mkazi wa Misufini Manispaa ya Morogoro kuhusiana na kauli ya kamishna huyo, amesema vitendo vya ukatili kwa wafungwa vipo sana.
“Mimi nimetumikia adhabu ya kifungo cha miaka mitano, nimeyaona mengi, askari kuwadunda wafungwa ni jambo la kawaida kwao, na wanapiga hasa. Na wanawafanyisha kazi ngumu sana wafungwa,” amesema Hamza.
Hata hivyo, amesema kama Serikali imeliona hilo inabidi ilifanyie kazi haraka, ili kunusuru maisha ya wafungwa magerezani wasiendelee kuteseka na kuhatarisha maisha yao.
Naye Khadija Abdul ambaye pia aliwahi kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili katika gereza moja jijini Dar es Salaaam na kwa sasa akiishi Kihonda Gorofani mjini hapa, amesema baadhi ya askari magereza ni wakatili kupita kiasi.
“Niliwahi kufungwa miaka miwili kati ya mwaka 2016 hadi 2018 na kipindi hicho kwenye gereza nililokuwa nimefungwa kuna wakati nilikuwa najikuta napigwa tu na askari bila sababu, tena wanakupiga kwa kukuchangia, wanafanya hivyo ili waogopwe, sasa kama magereza ni sehemu ya kurekebisha tabia kwa nini watu wapigwe tena kwa kuonewa?
“Namshukuru Mungu mpaka namaliza kifungo changu changu sikutoka na ulemavu licha ya kipigo nilichokuwa nakipata kutoka kwa maaskari tena wote wa kike na kiume hakuna hata mwenye huruma,” amesema.