Dar es Salaam. Serikali imesema bado inaendelea na uchunguzi katika kesi ya kuua bila kukusudia inayowakabili wanaodaiwa kuwa ni wamiliki watatu wa jengo lililoporomoka Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, wamedai upelelezi haujakamilika.
Washtakiwa hao ambao wote ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ni Leondela Mdete (49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam(61) mkazi wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour(38) mkazi wa Ilala.
Mdete na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya 31 ya kuua bila kukusudia katika kesi ya mauaji namba 33633/2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo, leo Jumatatu Februari 10, 2025, Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele akishirikiana na Eva Kassa ameieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini, kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
“Mheshimiwa hakimu, washtakiwa wote wapo mbele ya mahakama yako na kesi yao imeitwa leo kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amedai Mwakamele.
Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 10, 2025 itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.
Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao kinyume na kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Novemba 16, 2024 katika Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, washtakiwa hao isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha kifo cha Said Juma.
Katika shtaka la pili hadi la 31, washtakiwa hao siku na eneo hilo wanadaiwa kusabisha kifo cha Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu na Catherine Mbilinyi.
Vilevile, wanadaiwa kusababisha kifo cha Elton Ndyamukama, Mariam Kapekekepe, Elizabeth Kapekele, Hadija Simba, Frank Maziku, Rashid Yusuph, Ally Ally, Ajuae Lyambiro, Mary Lema na Khatolo Juma.
Pia, wanadaiwa isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusabisha kifo cha Sabas Swai, Pascal Ndunguru, Brighette Mbembela, Ashery Sanga, Venance Aman, Linus Hasara, Pascalia Kadiri, Issa Issa, Lulu Sanga, Happyness Malya na Brown Kadovera.