Benki itakavyodhibiti vikundi hewa mikopo asilimia 10

Dar es Salaam. Kuanza kutumia benki kama njia ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri nchini Tanzania imetajwa kuwa mwarobaini wa utoaji wa fedha kwa vikundi hewa uliokuwa ukitokea awali.

Hiyo ni kutokana na benki kuwa na ubobezi katika kufanya tathmini kujua uhalali wa kikundi, shughuli wanazozifanya na uwezekano wa kurejeshwa kwa fedha wanazoomba.

Hili limesemwa na wachambuzi wa masuala ya uchumi na biashara ikiwa ni siku tatu tangu benki ya CRDB kusaini mkataba wa kusimamia utoaji wa mikopo ya asilimia 10 katika halmashauri tano za Jiji la Dar es Salaam na Dodoma, Manispaa ya Kigoma, Halmashauri ya Mji wa Mbulu, na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Halmashauri hizi tano ni kati ya 10 ambazo zilitangazwa Aprili 16, 2024 kuwa zitatumika kufanya majaribio ya mikopo hiyo kupitia mfumo ulioboreshwa ambapo nyingine ni ile ya mji Newala, halmashauri za Wilaya ya Siha, Itilima na Bumbuli.

Mikopo hii kwa wanawake, vijana na wenyewe umelavu inarejea baada ya kusitishwa Mei 2023 na Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuwapo kwa utendaji usioridhisha unaofanya fedha nyingi kutorudi na uwepo wa vikundi hewa vilivyokopeshwa.

Inaanza kutolewa tena ikiwa ni baada ya kufanyika kwa maboresho yanayohusisha uanzishwaji wa kitengo cha usimamizi wa utoaji wa mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Jambo hilo lililoenda sambamba na uanzishwaji wa kamati ya usimamizi wa utoaji wa mikopo katika ngazi za Ofisi za wakuu wa mikoa, Halmashauri na Kata.

Miongoni mwa majukumu ya Kamati ngazi ya Kata ni pamoja na kutambua waombaji, kuthibitisha vikundi vya mikopo na kuvisajili katika mfumo mpya unaitwa Wezesha Portal na baada ya usajili Kamati itawasilisha ngazi ya Wilaya kwa hatua zaidi.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa), Dk Donald Mmari amesema uamuzi wa kutumia benki ni wa busara kwani awali kulikuwa na ufanisi mdogo.

Ufanisi hafifu ulionekana katika ukusanyaji wa fedha zilizotolewa au kutowafikia walengwa vizuri.

“Lakini benki wana uzoefu mkubwa katika utoaji wa mikopo ni jambo zuri kwani itasaidia kuongeza ufanisi. Wao hadi wakupe mkopo kuna taratibu za kibenki ambazo wanahakikisha wanazipitia ikiwemo kuwatambua wakopaji, miradi yao, sit u miradi ambayo imechambuliwa vuzuri ili kuhakikisha fedha wanayokupa inaweza kwenda kufanya kitu na kurejeshwa,” amesema.

Amesema jambo hilo linaongeza uwezekano wa kurejeshwa fedha kutokana na urahisi wa ufuatiliaji wa wateja inakuwa ni rahisi kuliko kutegemea watumishi wa halmashauri ambao wana majukumu mengine.

“Hii inakwenda kusaidia hata katika kudhibiti mikopo inayotolewa kwa vikundi hewa, kwani wanaweza kuthibitisha kuwa vikundi walivyopewa ni hai na siyo hewa, hii itafanyika kwa urahisi zaidi na kuondo mgongano wa kimaslahi,” amesema Dk Mmari.

Mmoja wa wakulima wa parachichi, Nestory Ayoub aliliambia mwanachi kuwa uamuzi wa kutumia benki ni mzuri lakini ulikuja kwa kuchelewa.

“Kwenye hela huwa hakuhitajiki maneno bali vitendo na mtu awe anajua anachokifanya vinginevyo utapata hasara, kitendo ca kutumia halmashauri kukopesha haukuwa umefikiriwa ipasavyo kwani hakukuwa na wataalamu wa kutosha kufanya tathmini za kina kabla ya kutoa hela,” amesema Ayoub na kuongeza.

“Wao waliwaza kufikisha malengo na kusifiwa wametoa hela nyingi kwa kinamama, vijana na wenye ulemavu lakini huku chini ufanisi wake ndiyo huu tunauona kupitia ripoti za ukaguzi.

Kuhusu uhafifu katika urejeshaji wa mikopo aliyozungumzia Dk Mmari, thamini iliyofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere inaonyesha hadi Juni 30, 2023, wanufaika wa mikopo katika mamlaka za serikali za mitaa 151 walikuwa hawajarejesha mikopo yenye jumla ya Sh79.7 bilioni.

Kupitiar ripoti kuu ya ukaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 mapitio ya mikopo iliyotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu yanaonyesha kuwa kuwa mamlaka za serikali za mitaa 46 zilikuwa na mikopo isiyorejeshwa ya jumla ya Sh5.7 bilioni kutoka kwa vikundi 1,334 vilivyositisha kufanya shughuli zao.

Pia ukaguzi huo ulionyesha kuwa vikundi 851 katika mamlaka za serikali za mitaa 19 vilivyoripotiwa kupokea mikopo ya jumla ya Sh2.6 bilioni havikuthibitika uwepo wake.

Kuhusu vikundi hewa, Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa akiwa katika hafla ya utiaji saini alisema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali viongozi wa mikoa na wilaya watakaobainika kuhusika katika utoaji wa mikopo kwa vikundi hewa.

“Fedha hizi ni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, hivyo lazima zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa. Wakuu wa mikoa na wilaya ambao wataruhusu uwepo wa vikundi hewa watawajibika moja kwa moja. Wananchi wanapaswa kuwa waaminifu kwa kurejesha mikopo yao ili mpango huu uwe endelevu,” alisema Mchengerwa.

Ameongeza zaidi ya Sh234 bilioni zinatarajiwa kutolewa kwa wananchi kupitia njia mbili: mikopo inayosimamiwa na benki katika halmashauri 10 na mikopo iliyoboreshwa katika halmashauri 174 nyingine.

Aidha, Mchengerwa alizitaka mamlaka za serikali za mitaa kuendelea kuchangia fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo hii kwa mujibu wa sheria ya fedha za serikali za mitaa.

“Katibu Mkuu, niletee orodha kama kuna halmashauri ambazo hazijachangia na zinadorora kuchangia na kama kuna halmashauri ambayo haijatekeleza ya maelekezo ya Rais,” amesema.

Ushauri wa Profesa Semboja

Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Haji Semboja amesema mbali na ufanisi kuonekana kupitia mfumo huu lakini ni vyema kukumbuka kuwa wanafanyabiashara wadogo wana changamoto mbalimbali za kimfumo ikiwemo kiuchumi, siasa, utamaduni ambazo huenda ndiyo zinaathiri shughuli zao.

“Wengine wanadhani hii ikitolewa ni kwa ajili ya serikali kujali wananchi wake wengine wanadhani kuwa ni wakati wa kuchukua fedha katika mfumo bila kuwajibika nazo, hii ndiyo kisiasa. Wengine wanachukua mikopo lakini ikitokea shughuli imegoma nyumbani kwake anahamisha matumizi hivyo masuala ya kijamii nayo yanachangia utendaji mbaya,” amesema.

Amesema wakati mwingine watu hawa wanakuwa wamechukua mikopo wakiwa na malengo mazuri lakini baadaye kunakuwa na matokeo ya vitu ambavyo vinakuwa nje ya uwezo wao jambo ambalo linawayumbisha.

“Benki inakuwa na uelewa mzuri wa masuala ya kifedha na itaonyesha ufanisi, kasoro zinaweza kuwapo lakini si sawa na vile ambavyo ilikuwa ikitolewa katika mfumo wa awali kwani vingi vitaweza kuendeshwa kwa ubobevu,” amesema.

Alipozungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa mpango huu unaendana moja kwa moja na jitihada zao kupitia programu ya IMBEJU inayolenga kuwainua wajasiriamali wadogo.

“Tutatoa elimu ya fedha, ushauri wa biashara, na kuhakikisha mikopo inawafikia walengwa kwa uwazi na ufanisi,” alisema.

Miongoni mwa vitu vilivyobadilika ni namna ambavyo mikopo hii sasa inatolewa kwa vikundi mbalimbali vinavyoomba.

Ili kuingia katika mchakato taratibu zinaonyesha kuwa ni lazima kikundi kitambulike na kupewa cheti cha utambuzi na halmashauri, kiwe kinachojishughulisha na shughuli za ujasiriamali mdogo au wa kati au kikundi kinachotarajia kuanzisha shughuli za ujasiriamali.

Pia kikundi cha wanawake na vijana kiwe na idadi ya wanakikundi kuanzia watano na kuendelea na kikundi cha watu wenye ulemavu kiwe na wanakikundi wasiopungua wawili.

Hata hivyo, kanuni ya 6a (1) ya utoaji mikopo hiyo inaeleza mtu mwenye ulemavu anaweza kuwa na sifa ya kupata mkopo kama kikundi cha watu wenye ulemavu endapo timu ya menejimenti ya halmashauri itajiridhisha kuwa amekosa mtu mwingine mwenye ulemavu wa kuungana naye katika eneo lake ila sifa nyingine zitafanana na zile za vikundi vingine.

Related Posts