Tanzania inavyofaidika na mikutano ya kimataifa

Dar es Salaam. Ukiachana na malalamiko ya msongamano wa magari na kufungwa kwa muda kwa baadhi ya barabara hususan jijini Dar es Salaam, mikutano mikubwa inayofanyika nchini ni nyenzo ya kusisimua uchumi unaolinufaisha taifa na hatimaye mwananchi mmoja mmoja.

Kwa mujibu wa wanazuoni wa uchumi na wadau wa utalii wa mikutano, changamoto zinazolalamikiwa inapotokea mikutano ni chache ukilinganisha na ukubwa wa faida inayopatikana kwa nchi na wananchi wake.

Mitazamo hiyo inakuja katika kipindi ambacho, Tanzania imekuwa mwenyeji wa mikutano kadhaa inayokusanya maelfu ya wageni wa kimataifa.

Hata hivyo, hatua ya kuwepo kwa mikutano hiyo si bahati mbaya, kwa kuwa Serikali ilishaweka wazi kuwa, katika mkakazi wa kupanua vipengele vya utalii, mikutano ni moja ya maeneo ya kipaumbele.

Miongoni mwa mikutano mikubwa iliyowahi kufanyika na itakayofanyika nchini katika siku za karibu ni ule wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati uliowakutanisha marais 20 wa mataifa ya Afrika.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na marais wa nchi za Afrika waliohudhuria mkutano wa nishati unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Pamoja na marais hao, wageni zaidi ya 2,000 kutoka nje ya nchi walihudhuria mkutano huo.

Mwingine ni mkutano wa kahawa unaotarajiwa kufanyika Februari 21 na 22, 2025 na utawakutanisha wadau zaidi ya 1,000 kutoka ndani na nje ya nchi.

Kama hiyo haitoshi, mkutano mwingine utafanyika Machi 5 hadi 7 mwaka huu, kuhusu petrol na utawakutanisha wadau wa sekta hiyo kutoka nchi zote za Afrika Mashariki.

Katika baadhi ya mikutano hiyo, kumeibuka malalamiko yanayotokana na kuwepo kwa msongamano wa magari na baadhi ya barabara kufungwa kwa muda, lakini wadau wanasema kinacholalamikiwa ni kidogo kuliko faida inayopatikana.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Februari 10, 2025 Mwanazuoni wa Uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi amesema mikutano hiyo inaleta biashara, inayosababishwa na huduma watakazohitaji wageni.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano wa nishati wakiwa kaitika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Mathalan, kwa ugeni wa marais, amesema huwa na wasindikizaji takriban 20 ambao wote watanunua bidhaa za nchini na kuhudumiwa kwa kutumia fedha zao.

Amesema watu hao hutumia fedha nyingi wakiwa ndani ya nchi, pia ni nafasi ya kukutana na fursa mbalimbali zilizopo Tanzania na hivyo wengine hurudi baadaye kwa utalii au uwekezaji.

Kwa mtazamo wa mchambuzi wa masuala ya biashara na uchumi, Oscar Mkude, mikutano hiyo katika sekta ya utalii ina faida ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja.

Kwa upande wa faida ya moja kwa moja, amesema washiriki hutumia huduma mbalimbali kama hoteli, chakula, usafiri wa ndani, lakini watanunua vitu vidogovidogo.

Kuhusu faida zisizo za moja kwa moja, amesema wageni kuona fursa zilizopo nchini na kuamua kuwekeza baada ya kuangalia mazingira ya biashara na soko lililopo.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli za Kitalii Tanzania (HAT), Kennedy Mollel amesema mikutano inayofanyika nchini ndiyo tafsiri halisi ya utalii wa mikutano.

Katika aina hiyo ya mikutano, amesema Watanzania wananufaika kwanza kwa kutoa huduma ambazo kwao ni biashara wanaingiza fedha kutoka kwa wageni wanaokuja.

Kwa mujibu wa Mollel, aina hiyo ya mikutano aghalabu huleta wageni wengi wanaolala katika hoteli na wanaonunua chakula na huduma nyingine na hivyo kuacha fedha nchini.

Yote hayo, amesema ni sehemu ya fedha inayoingia kwa Watanzania na inapokwenda kwenye mzunguko kila mwananchi atanufaika.

Katika huduma zinazotolewa, ameeleza wahudumu wanalipa kodi kwa Serikali na hivyo nchi inanufaika, hatimaye kila mwananchi ataguswa na manufaa husika.

Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)

Kennedy ameeleza manufaa mengine ni kwa Serikali kupitia ndege zake, kwa kuwa baadhi ya wageni watasafiri kwa ndege kuja nchini na wengine wakati wa kuondoka.

Mbali na hayo, alieleza ujio wa wageni unawapa nafasi ya kuitambua nchi, lakini wanaweza kushawishika ama kuwekeza au kwenda mbali zaidi na kuamua kutembelea vivutio vya utalii.

“Mambo yote hayo yanawanufaisha watoa huduma husika, Serikali kupitia kodi na hatimaye mwananchi mmoja mmoja kutokana na kodi itakavyotumika,” amesema.

Sambamba na hayo, amesema baadhi ya wageni wanaofika nchini wanakwenda kwenye maeneo ya mbali kusaka huduma za kawaida ambazo aghalabu hutolewa na wananchi wa kawaida.

Februari 21 na 22, 2025, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuwakaribisha wakuu wa nchi 25 za barani Afrika zinazozalisha kahawa katika mkutano wa tatu wa G-25 African Coffee Summit utakaofanyika JNCC, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huu unaoandaliwa na Wizara ya Kilimo utawakutanisha wadau zaidi ya 1000 wakiwemo wakuu wa nchi, viongozi wa kisekta, sekta binafsi, wakulima, waongeza thamani kwenye zao la kahawa, wataalamu, wafanyabiashara, wanawake, vijana na watumiaji wa kahawa kwa ujumla.

Machi 5 hadi 7, washiriki zaidi ya 1,000 kutoka nchi mbalimbali ikiwemo za Afrika ya Mashariki, wanatarajia kujifungia kwa siku tatu nchini kujadili mchango wa rasilimali za mafuta na gesi asilia katika maendeleo endelevu ya Afrika Mashariki na fursa za uwekezaji zilizopo.

Kupitia Maonyesho ya 11 ya Petroli ya Afrika Mashariki (11TH East African Petroleum Conference and Exhibition – EAPCE25), mkutano ukaozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan huku ukitanguliwa na mafunzo yanayotarajiwa kufanyika Machi 4, jijini hapa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema mkutano huo wa EAPCE25 utakaowaleta pamoja watunga sera, viongozi wa serikali kutoka nchi mbalimbali ikiwemo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wawekezaji wa kimataifa na wa ndani utakua na fursa mbalimbali.

“Pamoja na hayo kutakuwa na fursa za uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi, dhana ya kuelekea nishati safi, masuala ya mazingira, miundo ya kisera, kisheria na kiudhibiti katika mafuta na gesi na masuala mengine muhimu kwa sekta hiyo,” alisema.

Mkutano huu unatajwa kuwa fursa muhimu kwa wafanyabiashara kwani utahusisha maonyesho ya bidhaa na huduma kutoka kampuni mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi asilia.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano wa nishati wakiwa kaitika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Mwenyekiti wa Kamati ya Kikanda ya maandalizi ya EAPCE25 ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Nishati anayeshughulikia mafuta na gesi, Dk James Mataragio alisema mkutano huo utachangia mzunguko wa kifedha kwani utahusisha ziara za kitaaluma.

Alisema ziara zitafanyika katika maeneo ya kijiolojia katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuwapa washiriki mtazamo wa vitendo kuhusu sekta.

“Hili litawezesha wawekezaji na wadau kubaini fursa za biashara na ushirikiano katika sekta ya nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema Dk Mataragio.

Related Posts