Hamdi abanwa jeshini, Yanga yaangusha pointi

MBINU za makocha Ahmad Ally (JKT Tanzania) na Miloud Hamdi (Yanga) zimeonekana kutoshana nguvu katika dakika 45 za kwanza wakati timu hizo zilipopambana kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar.

Hamdi ambaye alikaa kwa mara ya kwanza kwenye benchi la Yanga kuiongoza timu hiyo katikq mechi ya ligi tangu atambulishwe Februari 4, 2025, alishuhudia dakika 45 timu yake ikishindwa kupenya ngome ya JKT Tanzania na matokeo kuwa 0-0.

Juhudi za washambuliaji wa Yanga, Prince Dube na Clement Mzize kulishambulia lango la JKT Tanzania, zilizimwa na walinzi wa kati, nahodha Edson Katanga aliyekuwa akishirikiana vema na Wilson Nangu huku kipa Yakubu Suleiman akiwa imara langoni.

Eneo la kiungo cha kati la JKT Tanzania lilionekana kuyumba hasa kwenye ukabaji hali iliyomlazimu Kocha Ahmad Ally wakati kipindi cha pili kikitaka kuanza alimtoa Ally Msengi na kuingia Edward Maka, huku pia akiimarisha ulinzi wa kulia akimtoa George Wawa nafasi yake akachukua Salum Khamis Salum.

Kabla ya mabadiliko hayo, JKT Tanzania ilionyesha ukomavu wa kushambulia na kuzuia huku kipa Yakubu Suleiman akiokoa nafaso ya wazi ambayo Mzize ilibaki kidogo afunge dakika ya 45 na kuwa kona ya kwanza ya mchezo huo.

JKT Tanzania wamekuwa wagumu wanapocheza uwanja wao wa nyumbani kwani rekodi zinaonyesha kabla ya mchezo wa leo ilikuwa haijapoteza ikishinda tatu na sare nne, ikifunga mabao saba na kuruhusu matatu, ikiondoka na cleansheet tano.

Yanga ambayo ilikuwa inapambania pointi tatu za kuwafanya kukaa kileleni kwa amani, ilikuwa inaifukuzia rekodi yake ya kushinda mechi zote za ugenini kwenye ligi msimu huu baada ya kucheza saba kabla ya kukutana na JKT Tanzania ikifunga mabao 12 na haijaruhusu, clean sheet zikiwa saba.

Katika kukutana kwao tangu msimu wa 2018-2019, kabla ya leo Yanga ilikuwa imeshinda 7 na kufunga mabao 18, sare zikiwa 2, wakati JKT haijashinda ikifunga mabao 3.

Mara ya mwisho timu hizi kucheza uwanjani hapa ilikuwa Aprili 24, 2024 na matokeo yakawa suluhu 0-0. Mechi tano za mwisho JKT ilikuwa haijafunga bao dhidi ya Yanga, mara ya mwisho ilifunga bao Juni 17, 2020 katika sare ya 1-1

SHUGHULI ILIKUWA PEVU
Mchezo ulitawaliwa na matukio mengi ya kuchezeana kwa nguvu lakini ilishuhudiwa kipindi cha kwanza licha ya kufanyika jumla ya faulo 20, lakini mwamuzi Ahmed Arajiga hakuonyesha kadi yoyote.

Miongoni mwa matukio ya kushangaza ni namna walinzi wa JKT Tanzania walivyokuwa wakomkaba Dube na kumsababishia kubadili jezi mapema dakika ya nane baada ya ile ya kwanza kuchanika.

Kipindi cha pili, mwamuzi Arajiga alikuwa mkali kwani dakika 25 za kwanza aliwaonyesha kadi za njano wachezaji wanne, Salum Khamis Salum, Hassan Maulid Nassoro na Wilson Nangu wa JKT Tanzania sambamba na Kennedy Musonda.

VIKOSI
JKT TANZANIA: Yacoub Suleiman, George Wawa/Salum Khamis, Karimu Mfaume, Edson Katanga, Wilson Nangu, Ally Msengi/Maka Edward, Najim Maguru, Hassan Maulid, Gamba Matiko, Hassan Dilunga/Ismail Aziz na Jafary Maneno/Said Ndemla.

YANGA: Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Hamad, Khalid Aucho, Clement Mzize/Kennedy Musonda, Mudathir Yahya, Prince Dube, Clatous Chama/Aziz Ki na Pacome Zouzoua/Maxi Nzengeli.

Related Posts