NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
WANAHARAKATI wa Jinsia na Maendeleo (GDSS) wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Maji kutekeleza kikamilifu bajeti waliyotenga ili kukidhi mahitaji kwa jamii nzima hasa kwa wakina mama ambao wamekuwa waathirika namba moja katika utafutaji wa maji.
Hayo yamebainishwa leo, Mei 15,2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa semina za Jinsia na Maendeleo zinazofanyika kila Jumatano katika ofisi za TGNP -Mtandao, ambapo wamechambua bajeti ya Wizara ya maji na kugundua udhaifu katika bajeti hiyo.
Akizungumza katika semina hizo Mwanaharakati wa masuala ya Jinsia Bi.Agness Lukanga amesema kulingana na bajeti kuwepo lakini utekelezaji bado haukidhi mahitaji ya jamii kwani katika maeneo mengi wakina mama wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata maji jambo ambalo ni hatarishi.
“Serikali inatakiwa kutekeleza bajeti kama walivyopanga ili kuwapunguzia wakina mama majukumu ya utafutaji wa maji kwani wao ndo wanaonekana ndo wanaathirika kwa kiwango kikubwa katika ukosefu wa maji”. Amesema
Kwa Upande wake,Mwanaharakati Kutoka Kituo Cha Taarifa na Maarifa kata ya Majohe Bi.Winfrida Haraka, amesema kuwa kuna maeneo mengine mabomba ya majisafi yamewafikia, lakini upatikanaji wa maji kwenye maeneo hayo ni hafifu kutokana na kukatwa mara kwa mara.
Amesema miundombinu mibovu ya majisafi pia uchangia ukosefu wa majisafi katika maeneo ambayo mabomba ya maji yamepita kwani kuna wakati maji yakifunguliwa hayawafikii wahusika kutokana na mabomba kupasuka.
Nae Mwanaharakati kutoka Kituo Cha Taarifa na Maarifa kata ya Mburahati Bw.Alan Luyeje,amesema maji salama ni hitaji la msingi kwa jamii nzima ambapo katika usafi wa mwanamke ni muhimu hata katika sehemu za mikusanyiko hasa hospitali na shule yanahitajika zaidi kwa ajili ya usafi na afya
Pamoja na hayo wadau hao wa semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) wameiomba serikali kujenga mfumo Shirikishi kwa wananchi kushiriki katika mchakato wa kuandaa bajeti kabla ya kupitishwa bungeni ambayo itasaidia kukidhi mahitaji ya jamii