Nimesoma tamko la pamoja (communique), kutoka kwa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini ya Afrika (SADC), kuhusu mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Februari 8, 2025.
Upande mwingine nilivutiwa na simulizi ndefu kuhusu mgogoro wa DRC na hatua zake za utatuzi iliyotokewa na mwanadiplomasia, Balozi Liberata Mulamula, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kutoka wakuu wa EAC na SADC, hadi Balozi Mulamula, hadithi ni moja ila haikidhi.
Mgogoro wowote lazima uwe na wahusika wakuu. Inawezekana pia kukawa na wahusika wadogo. Ili kuelewa msingi wa mgogoro, ni muhimu kutambua wahusika wote.
Kuhusu DRC, nilifuatilia mkutano baina ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame, na waandishi wa habari, uliofanyika Februari 2, 2025. Maeneo yote matatu, kikundi cha M23 kinatajwa utadhani ni muhusika mkuu wa mgogoro unaoendelea sasa. Na hii ni kwa sababu za kihistoria.
Ni kweli, kihistoria, M23 au Machi 23, ni muhusika mkuu wa ghasia zilizopo Mashariki ya DRC, hasa jimbo la Kivu Kaskazini (Goma), ingawa hufika hadi Kivu Kusini (Bukavu), palipo na jamii ya Wnyamulenge (Watutsi).
Mgogoro wa sasa ni muhimu kuzingatia historia kwani inahusika, lakini upo ukweli usiosemwa, ama kwa bahati mbaya au kwa makusudi. Kwa sasa, M23 ndiye muhusika mkuu. Shida iliyopo ni kwamba M23 wameungana. Ni muungano wa pande mbili zenye masilahi yasiyofanana lakini wanachangia adui.
M23 wanafahamika. Malengo yao ni kupigania haki za jamii ya Watutsi waliopo DRC. Wanataka watambulike kama raia wa DRC na wapate haki na stahiki zote kama wananchi halali wa nchi hiyo. Kutokana na madai haya, M23 ni mnyororo unaounga hadi miaka 65 iliyopita, kabla DRC haijapata uhuru.
Watutsi wa DRC wapo katika historia ya mapambano ya uhuru wa nchi hiyo. Walishirikiana na Mobutu Sese Seko katika misheni yake ya kutwaa madaraka, kisha akawageka, akapitisha sheria inayosema Watutsi wa DRC siyo raia wa nchi hiyo, ambayo aliita Zaire.
Miaka yote 32 ambayo Mobutu aliiongoza Zaire (DRC), alikuwa vitani na Watutsi hao. Kisha, Watutsi hao walishirikiana na Laurent Kabila kumwondoa Mobutu wakati wa Vita ya Kwanza ya Congo, maarufu kama Vita ya Banyamulenge. Jamii ya Watutsi wa DRC Kivu Kusini huitwa Wanyamulenge (Banyamulenge).
Watutsi wa DRC walikuwa sababu ya Vita ya Pili ya Kongo, pale Wanyamulenge walipoona wamegeukwa na Kabila na kuingia vitani kumkabili. Katikati ya mapambano dhidi ya Kabila, kikazaliwa kikundi cha CNDP, kilichobadili jina kuwa M23.
Hili halibishaniwi kuwa M23 ni mhusika msumbufu katika DRC. Wanachopigania ni haki ya kimsingi.
Serikali ya DRC, kutoka Mobutu, Kabila mkubwa, mwanaye, Joseph Kabila hadi Rais wa sasa, Felix Tshisekedi, wanataka Watutsi wa DRC watambulike kama Wanyarwanda.
Inapotajwa Rwanda, ndipo Kagame anasema anawaunga mkono Wanyamulenge na Watutsi wa DRC Kivu Kaskazini kwa kuwa ni raia wa DRC, hivyo wanastahili kupata haki yao ya uraia.
Zaidi ya Watutsi 400,000 wa DRC wanaishi kwenye kambi za wakimbizi Rwanda na Uganda.
Ukiuendea ukweli kama ulivyo, mgogoro wa sasa wa DRC, mhusika mkuu ni Muungano wa Mto Congo au kwa Kiingereza wanajiita “Congo River Alliance”. Ni mkusanyiko wa vikundi vya uasi DRC, vinavyoongozwa na Corneille Nangaa.
Inakadiriwa kuwa vikundi takriban 20 au zaidi vya uasi DRC vimeungana na sasa vinaunda Muungano wa Mto Kongo, ambao kiongozi wake ni Nangaa. Moja ya vikundi hivyo ni M23.
Hiyo maana yake ni kuwa pande zinazohusika, Muungano wa Mto Congo ndiye muhusika mkuu kwenye mgogoro wa sasa kwa upande mmoja, halafu Serikali ya DRC upande wa pili. M23 ni kundi dogo sana.
Kama mgogoro wa DRC ungekuwa filamu, Muungano wa Mto Congo na Serikali ya DRC wangeweza kuwa wahusika wakuu, na M23 ingepewa hadhi ya wahusika washiriki.
Tatizo ni kwamba mijadala mingi, ikiwemo ya communique ya wakuu wa EAC na SADC, haizungumzii Muungano wa Mto Congo, isipokuwa M23.
Moja ya makubaliano ya wakuu wa EAC na SADC ni kufanya mazungumzo na M23. Hili ni kosa. Mgogoro wa DRC wa sasa haupo kihistoria, isipokuwa historia imekutana na masilahi mapya. M23, kila wakati, wamekuwa wakipigania masilahi ya maeneo wanayoishi Watutsi wa DRC, lakini mgogoro wa sasa hauegemei Watutsi pekee (Wanyamulenge), bali ni vita ya madaraka.
Uhusika wa Nangaa unapaswa kuamsha hisia za wengi kuhusu masilahi ya mgogoro wa sasa. Nangaa hatokani na jamii yoyote ya Watutsi, wala asili yake siyo Mashariki ya DRC. Nangaa anatokea jimbo la Haut-Uele, lililopo Kaskazini ya DRC, jirani na mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
M23, siku zote masilahi yao ni Mashariki ya DRC, jimbo la Kivu Kaskazini, wakiutazama zaidi mji wa Goma, wakati Wanyamulenge macho yao ni Kivu Kusini, mji wa Bukavu.
Majimbo hayo mawili, yanapakana na Rwanda. Majimbo ya Mashariki ya DRC yana utajiri mkubwa wa dhahabu, tin, tungsten, tantalum. Madini hayo yanayopatikana kwa wingi Mashariki ya DRC huunda kitu kinachoitwa 3TG. Maana yake, 3T au T tatu ni herufi za mwanzo za tin, tungsten, na tantalum, wakati G ni dhahabu (gold).
3TG huitwa madini ya mgogoro, maana ni sehemu ya kiini cha machafuko DRC. Tin, tungsten, tantalum, na dhahabu hutumika kutengeneza simu za mkononi, magari, na vito vya thamani. Ukweli ni kwamba yanakopatikana, damu inamwagika kwa wingi.
Malalamiko ya Serikali ya DRC ni kwamba Kagame anawaunga mkono M23 na vikundi vingine Mashariki ya DRC ili kutengeneza mwanya wa kupora madini, kwamba Rwanda inajengwa kwa madini ya DRC.
Ukitaka kugusa kiini halisi cha mgogoro wa sasa wa DRC, lazima urejee Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Desemba 30, 2018.
Nangaa alikuwa Rais wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (Ceni). Ndiye mtuhumiwa mkuu wa udanganyifu wa matokeo ambayo Tshisekedi alitangazwa mshindi.
Emmanuel Shadary alikuwa mgombea aliyeungwa mkono na Rais aliyekuwa madarakani, Joseph Kabila. Mchuano ukawa kati ya Shadary na Kiongozi wa upinzani, Martin Fayulu. Dunia ilishangazwa na Nangaa alimtangaza Tshisekedi kuwa mshindi wa urais.
Minong’ono na tuhuma zikawa, kwamba Kabila kupitia Nangaa alicheza karata ya mazingaombwe, kumtangaza Tshisekedi mpinzani kuwa mshindi ili kunyamazisha wapinzani wengine.
Tshisekedi akawa Rais asiye na nguvu, hakuwa na wabunge. Ikabidi aongoze serikali kwa kushirikiana na chama cha Kabila, PPRD. Baada ya mwaka mmoja na siku 232, ndoa ya Tshisekedi na PPRD ilivunjika.
Kipindi ndoa ya Tshisekedi na PPRD (Kabila) inavunjika, ndiyo muda ambao Nangaa alikuwa anaondoka Ceni, kisha swahiba wa Tshisekedi, Denis Kazadi kadima, alichukua usukani. Baada ya Nangaa kuondoka Ceni, alitoboa siri ya makubaliano baina ya Tshisekedi na Kabila.
Kisha, Nangaa alianzisha chama cha siasa, ADCP (Hatua kwa ajili ya Utu wa Kongo na Watu Wake). Nangaa kupitia ADCP, alijipanga kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu DRC 2023. Alipanga pia chama hicho kishiriki uchaguzi ngazi zote. Aliponusa mpango wa kufunguliwa mashitaka ya udanganyifu wa kura mwaka 2018, Nangaa alikimbilia Nairobi, Kenya.
Agosti 2023, Nangaa akiwa Nairobi, alitangaza kuanzishwa kwa Muungano wa Mto Congo (AFC). Desemba 15, 2023, M23 walisaini makubaliano ya kujiunga AFC. Utiaji saini huo na tamko kuwa M23 imejiunga AFC vyote vilifanyika Nairobi.
AFC, malengo yao ni kumwondoa madarakani Tshisekedi, wakati M23 wanapigania haki ya Watutsi wa DRC. Ndoa isiyotakatifu imeundwa kwa masilahi ya aina tofauti. AFC wameona M23 kuwa ni mshirika muhimu katika kutimiza malengo yao ya kumpindua Tshisekedi. M23, wamepata nguvu kubwa.
Maana yake ni kuwa walioiteka Goma ni AFC, siyo M23, sawa na miji mingine ya Minova, Sake, Rutshuru, Nyiragongo, Masisi, na Nyabibwe. M23 kwa sasa ni tawi la AFC (Muungano wa Mto Kongo). Kila kitu kuhusu amani ya DRC, lazima kihusishe AFC kwanza, kisha M23 ifuate.
Tshisekedi anakuwa sawa na mwenye kutapatapa. Kuna wakati anamtaja Kabila kuwa kiini cha machafuko Mashariki ya DRC, wakati huohuo anamtuhumu Kagame.
Tshisekedi hasemi uongo, wote ni wahusika. Kagame anawaunga mkono M23, lakini kikundi hicho hakijawahi kuwa na dhamira ya kutoka Mashariki, Kivu Kusini, na Kivu Kaskazini, kuelekea Magharibi, ilipo Kinshasa, mji mkuu wa DRC, na kuipindua serikali.
Tshisekedi anajua wazi kwamba vita ya sasa DRC inatokana na yeye (Tshisekedi) kikiuka makubaliano haramu, kipindi anakabidhiwa nchi Januari 2019, baada ya mazingaombwe ya Kabila na Nangaa katika Uchaguzi wa Desemba 30, 2018.
Nangaa na wenzake hawapiganii masilahi madogo, kama kushika majimbo ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini kama M23, wao wanataka kutwaa nchi nzima kutoka Mashariki hadi Magharibi, kwa kushika Kinshasa na serikali yote. Uwepo wa Nangaa kwenye misheni ya AFC kama kiongozi, ndiyo inamfanya Tshisekedi amtaje Kabila. Huu siyo uongo.
Mgogoro wa DRC wa sasa pengine usingekuwepo kama wakuu wa EAC na SADC wangesimama kidete ili haki itendeke kwenye Uchaguzi Mkuu wa DRC 2018. Waliacha Kabila, Nangaa, na Tshisekedi watengeneze makubaliano haramu, sasa wamegeukana, na matokeo yake kila lawama inajazwa kwa M23, wakati wao wamealikwa kwenye vita ya wakubwa.