VIDEO: Mahakama ilivyosikiliza maelezo anayedaiwa kumua mumewe

Moshi. Upande wa mashitaka, katika kesi ya mauaji yanayomkabili mkazi wa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Beatrice Elias Kway (36) anayedaiwa kumuua mumewe nyumbani kwa mzazi mwenzake, Ephagro Michael Msele (43) umeeleza hatua kwa hatua mauaji hayo yalivyotokea.

Mfanyabiashara huyo maarufu mjini hapa, anadaiwa kuuawa usiku wa Mei 25, mwaka 2024 katika Kitongoji cha Pumuani A, wilayani hapa baada ya mshitakiwa huyo kudaiwa kumvizia mumewe huyo akiwa nyumbani kwa mzazi mwenzake na kisha kumshambulia kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni kisu.

Kwa mara ya kwanza mshitakiwa huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Juni 10, 2024,  akikabiliwa na kesi ya mauaji namba 15731 ya mwaka 2024 , mbele Hakimu Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Herieth Mhenga na kusomewa mashitaka yake na mwendesha mashitaka wa Serikali, Henry Daudi.

Akisoma maelekezo ya awali (PH) leo, Februari 10, 2025, mwendesha mashitaka wa Serikali, Grace Kabu, mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Jaji Safina Simfukwe, amedai kuwa Mei 25, 2024 mshitakiwa huyo alimuua kwa makusudi mwenza wake baada ya kumfuata mumewe nyumbani kwa mzazi mwenzake.

Amedai kuwa, siku hiyo ya  tukio saa 2:30 usiku mshitakiwa huyo,  alikwenda eneo la tukio baada ya kumfuatilia marehemu na kumkuta akitoka nyumba ya Idda Sebastian Massawe, mwanamke ambaye alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na marehemu.

“Baadhi ya hapo mshitakiwa alianza kugombana na marehemu na wakati wanagombana mshitakiwa alimchoma kisu na hapo hapo  alipoteza nguvu na kuanguka chini,” amedai mwendesha mashitaka huyo.


Mahakama ilivyosikiliza maelezo anayedaiwa kumua mumewe

Amedai kuwa, baada ya tukio hilo kutokea, mshitakiwa alipiga kelele na ndipo alijitokeza mwenyekiti wa kitongoji hicho pamoja na baadhi ya majirani wa eneo hilo.

Ameeleza kuwa, baada ya mwenyekiti kufika eneo la tukio  alitoa taarifa polisi na polisi walifika eneo la tukio ambapo walichunguza mwili wa marehemu na kumkuta akiwa na jeraha la kuchomwa na kitu chenye ncha kali mgongoni na ndipo walipoanza kufanya upekuzi eneo la tukio kutafuta kisu kilichotumika kumchoma marehemu.

“Wakati wakichunguza mwili wa marehemu, kaka wa marehemu aitwaye Israel Msele aliwataarifu polisi kuwa baadhi za mali za marehemu anazo mshitakiwa,”

Pia, alidai mshitakiwa aliwaambia polisi kuwa, alichukua simu moja aina ya iphone na kuiweka katika pochi yake ambayo pochi hiyo aliwapa marafiki zake ambao walifika eneo la tukio baada ya mshitakiwa kutoa taarifa.”

Aidha, alidai kuwa, polisi walitaka Mshitakiwa akabidhi pochi hiyo na walipofanya upekuzi ndani ya pochi hiyo, walikuta power bank moja ambayo ilikuwa na alama ya damu, kisu kimoja ambacho kilikuwa na alama ya damu na mabando mawili ambayo yalikuwa na fedha taslimu.

“Bando moja lilikuwa na thamani ya Sh505,000 na bando jingine lilikuwa na Sh 379,000 na baada ya upekuzi huo hati ya kukamata vielelelezo ilijazwa na kusainiwa na mashahidi walioshuhudia upekuzi huo,”

Amedai kuwa, baada upekuzi huo kufanyika, mshitakiwa alikamatwa na mwili wa marehemu ulichukuliwa eneo la tukio na kupelekwa hospitali ya Rufaa ya  Kanda Kaskazini, KCMC.

Hata hivyo, amedai kuwa, Mei 27, 2024 mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi wa kitabibu katika hospitali hiyo, na taarifa ya uchunguzi ilionyesha kuwa, chanzo cha kifo cha marehemu kilitokana na kuvuja damu nyingi kutokana na jeraha alilopata kwenye mapafu.

“Vile vile kisu ambacho kilikuwa na alama za damu, fulana ya kata mikono, t-shirt ya marehemu pamoja na sampuli ya damu kutoka kwenye mwili wa marehemu, ‘power bank’ moja ambayo ilikuwa na alama za damu,  sampuli ya damu iliyokaushwa kutoka eneo la tukio, sampuli ya kinywa pamoja na sampuli ya damu zilizochukuliwa kwa mshitakiwa, pochi moja ambayo ilikuwa na alama za damu, ndani yake pamoja na nguo ya kike ambayo ilikuwa na alama ya damu vyote vilipelekwa kwenye maabara ya mkemia mkuu wa Serikali Dar es salaam kwa ajili ya uchunguzi wa vina saba (DNA).

“Baada ya uchunguzi wa maabara kufanyika mpangilio wa vina saba, kisu kilichokutwa na alama za damu zimeoana na mpangilio wa vina saba katika nguo ya marehemu, sampuli ya damu iliyochukiliwa katika mwili wa marehemu, power bank moja ambayo ilikuwa na alama ya damu pamoja na pochi ambayo ilikuwa na alama ya damu,”

“Vile vile mpangilio wa vina saba katika kisu ambacho kilikuwa na alama ya damu ulioana na mpangilio wa vina saba kutoka katika sampuli ya kinywa na damu iliyochukuliwa kutoka kwa mshitakiwa,” amedai mwendesha mashitaka huyo.

Amedai kuwa, mshitakiwa alipohojiwa katika maelezo yake alikataa kutenda kosa hilo na baadaye alifikishwa mahakamani kwa kosa la kuua kwa kukusudia.

Hata hivyo, baada ya kusomewa maelezo hayo mshitakiwa huyo alipoulizwa na Jaji Simfukwe kama maelezo hayo ni sahihi, mshitakiwa huyo alikri kuwa majina yaliyotajwa katika kesi hiyo ni yake na kwamba aliyefariki ni mume wake na waliishi kwenye ndoa miaka 18 na wana watoto 6.

“Majina yaliyotajwa ni yangu, ni kweli nilikamatwa na polisi Mei 25, 2024  na marehemu ni mume wangu wa ndoa na tulikuwa na miaka 18 ya ndoa,”alieleza mshitakiwa huyo

Mashahidi/Vielelezo vitakavyotumika katika kesi hiyo

Mwendesha mashitaka huyo wa Serikali, ameeleza mahakama hiyo kuwa katika kesi hiyo kutakuwa na vielelezo saba ambavyo ni nyaraka na vitano ambavyo ni vielelezo halisi pamoja na mashahidi 16.

Akiahirisha kesi hiyo, Jaji Simfukwe amesema, shauri hilo litapangiwa tarehe ya usikilizwaji na Naibu Msajili wa mahakama hiyo na pande zote zitajulishwa.

“Wakati wa kusubiri tarehe ya kusikiliza kesi hii mshitakiwa utaendelea kukaa mahabusu,”amesema Jaji Simfukwe

Related Posts