Iringa. Wafanyabiashara wa vitunguu maji mkoani Iringa wamelalamikia kupanda kwa bei ya zao hilo kutoka Sh60,000 hadi kufikia kati ya Sh140,000 na Sh180,000 kwa gunia moja.
Wafanyabiashara hao wameeleza kuwa kwa sasa vitunguu maji shambani vinauzwa Sh180,000 ikilinganishwa na bei ya Desemba 2024 ya Sh70,000 kwa gunia na Sh 160,000, bei ya Januari hadi Februari 2025 wiki ya kwanza.
Wafanyabiashara hao kutoka Soko Kuu la Manispaa ya Iringa wameyasema hayo leo Februari 10, 2025 wakati wakizungumza na Mwananchi ambapo wamefafanua kuwa mabadiliko hayo ya bei yamekuwa changamoto kwa wateja sokoni kutokana na uuzaji mdogo wa bidhaa.
Aidha, baadhi ya wafanyabiashara wa vitunguu Iringa wamesema kuwa ongezeko hilo la bei limetokana na hali ya unyeshaji wa mvua kwani zao hilo halihitaji mvua nyingi, hivyo wakulima wengi kwa sasa hawalimi na ambao wana vitunguu ndio wanauza bei ya juu.
Mmoja wa wafanyabiashara wa vitunguu maji kutoka Soko Kuu la Manispaa ya Iringa, Emmanuel Tishu ameeleza kuwa ongezeko la bei limekuwa ni fursa nzuri kwa wakulima kwani walikuwa wakikumbwa na changamoto za kupata faida kubwa kutokana na bei ndogo ya zamani.
“Kwa sasa biashara ya vitunguu ipo juu sana na vitunguu hivyo tunachukulia vijiji vya mbali, mfano Idodi, Mgama, Ruaha mbuyuni na Pawaga ambapo tukinunua gunia Sh140,000 tunauza kisado cha lita moja Sh2,000 wakati bei ya zamani ilikuwa ni Sh1,000,” amesema Tishu.
Kwa upande mwingine, wafanyabiashara hao wamesema kwa sasa changamoto kubwa inabaki kuwa upatikanaji wa vitunguu vya kutosha kutokana na baadhi ya wakulima kuficha vitunguu kwa kuamini kuwa bei unaweza ikapanda zaidi ya hapo na ikaja kuwalipa zaidi.

Wafanyabiashara hao wameongeza kuwa licha ya ongezeko la bei, changamoto nyingine inabaki kuwa usafirishaji wa mazao hayo kutoka mashambani hadi sokoni ambapo gharama za usafiri zimepanda.
Baadhi ya wakulima wa vitunguu kutoka maeneo tofauti tofauti mkoani Iringa, wameeleza kwamba kupanda kwa bei hiyo kumewapatia fursa nzuri kwa wale ambao waliwekeza katika kilimo hicho kutokana na bei nzuri ambayo wanauza sasa hivi.
Vilevile, wakulima hao wameeleza kuwa bado uwepo wa mvua bado ni kikwazo kwa baadhi ya wakulima kwani zao hilo haliitaji mvua nyingi hivyo mara kwa mara zao hilo limekuwa likiozea shambani na kupata hasara.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi kutoka mkoani Iringa ambao ni walaji wa zao hilo wamekiri kuwa ongezeko hilo la bei limesababisha kupata bidhaa ndogo kwa gharama kubwa kitu ambacho kinasababisha muda mwingine kutotumia kiungo hicho katika mapishi mbalimbali.
Wananchi mkoani Iringa ambao ni walaji wa vitunguu, wamesema ongezeko kubwa la bei ya zao hilo limeathiri matumizi yao ya kila siku na kuwaathiri kiuchumi.
Aidha, wengi wao wamesema kwa sasa wanalazimika kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kununua vitunguu maji, jambo ambalo limefanya baadhi yao kupunguza matumizi ya kiungo hicho katika mapishi yao.
Asha Nzalalila, mkazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, ameeleza namna kupanda kwa bei ya vitunguu kulivyoathiri maisha yake ya kila siku katika matumizi ya nyumbani.
“Kwa sasa tunapata vitunguu kwa bei kubwa, na mara nyingi tunashindwa kutumia kama zamani, hivyo mara nyingi tunapata vitunguu vidogovidogo kutokana na bei yake kupanda,” amesema Asha.
Ikumbukwe kuwa kupanda kwa bei za kitunguu maji katika mkoa wa Iringa kwa mwaka 2025 si mara ya kwanza kwani Januari, mwaka 2015, zao hilo lilipanda na kuwa Sh70,000 na Sh160,000 huku sasa ikiwa ni Sh 180,000 ukilinganishaa na bei iliyozoeleka ya kati ya Sh40,000 na Sh60,000 kwa ujazo wa gunia moja.