Manyara. Wananchi wa Kata ya Kia (Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro), Kata ya Majengo (wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha), na Kata ya Naisinyai (wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara) wameandamana kushinikiza Serikali kutatua changamoto zinazowakabili, ikiwemo eneo korofi linalosababisha mafuriko mara kwa mara.
Kwa mujibu wa wananchi hao, mafuriko hayo yamesababisha vifo, majeruhi, na uharibifu wa mali pamoja na mazao ya chakula wanayolima katika maeneo hayo.
Baadhi ya wananchi kutoka wilaya za Arumeru, Simanjiro na Arumeru wakiwa wamefunga Barabara ya Mirerani hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), wakishinikisha Serikali kutatua changamoto ikiwemo eneo korofi linalosababisha mafuriko kwenye mashamba na makazi yao. Picha na Janeth Mushi
Wamesema maji hayo yanatoka kwenye mito mitatu, ikiwemo Mto Kikuletwa, na hukusanyika sehemu moja, lakini kutokana na miundombinu isiyo rafiki, maji hayo hukwama kwenye kingo za barabara na kusababisha mafuriko.
Wananchi hao wameandamana na kufunga barabara kwa saa nne, kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa 2:44 asubuhi ya leo, Jumanne Februari 11, 2025, katika eneo la Kijiji cha Naisinyai, mpakani mwa wilaya hizo. Barabara hiyo ni njia kuu inayounganisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na machimbo ya madini ya Tanzanite huko Mirerani.
Licha ya jitihada za viongozi wa maeneo hayo, wakiwemo madiwani, viongozi wa mila, na askari wa Jeshi la Polisi, kuwaomba wananchi kupisha barabara, waligoma na kuendelea kushikilia mabango yenye ujumbe mbalimbali. Miongoni mwa mabango hayo, baadhi yalisomeka: “Ni miaka mitatu sasa wananchi hawalimi kutokana na mafuriko.”
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amir Mkalipa, alipofika eneo hilo na kuzungumza na wananchi, amewataka kufungua barabara ili kuruhusu abiria waliokwama waendelee na safari zao.
Aidha, Mkalipa amewaeleza wananchi kuwa kesho, Jumatano, kutafanyika kikao cha pamoja kati ya wakuu wa wilaya hizo tatu (Hai, Simanjiro, na Arumeru), madiwani, na wenyeviti wa vijiji husika kwa lengo la kujadiliana na Bonde la Pangani kuhusu utatuzi wa tatizo hilo.
Endelea kufuatilia Mwananchi.