KATIKA kuhakikisha ile Gusa Achia Pro Max inafanya kazi ipasavyo, kocha mpya wa Yanga, Miloud Hamdi ameongeza dozi kwa mastaa wa timu hiyo.
Achana na mazoezi ya kabla ya mechi wanayoyafanya wakiwa Avic Town au wakati mwingine KMC Complex, dozi imeongezwa katika mazoezi muda mfupi baada ya mechi.
Yanga imekuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi muda mfupi baada ya mechi kumalizika ambapo kwa kawaida hutumia takribani dakika 10 mpaka 15. Msimu huu imefanya hivyo chini ya Miguel Gamondi kisha Sead Ramovic akaendeleza alipochukua mikoba yake Novemba 15, 2024 kabla ya kusepa Februari 4, 2025.
Jambo jipya alilokuja nalo Miloud Hamdi aliyetambulishwa Februari 4, 2025 ni muda wa mazoezi yanayofanyika baada ya mechi na wanaohusika.
Wakati wa Gamondi na Ramovic, baada ya mechi wachezaji waliohusika kufanya mazoezi hayo ni wale walioanzia benchi pekee lakini waliocheza kikosi cha kwanza hata kama hawakumaliza mechi hawahusiki. Mechi ikiisha walikuwa wakibadilisha nguo na kuondoka wakiwaacha wenzao wakipambana.
Mara kadhaa imeshuhudiwa kocha wa viungo, Taibi Lagrouni (kipindi cha Gamondi) na Adnan Behlulovic (kipindi cha Ramovic) ndio waliokuwa wakisimamia mazoezi hayo yaliyokuwa yakidumu kwa takribani dakika 10 mpaka 15 baada ya mechi.
Mazoezi hayo ni ya kuweka miili sawa kwa kukimbia, kuchezea mpira na kunyoosha viungo.
Hamdi ambaye leo Februari 10, 2025 ameiongoza Yanga kwa mara ya kwanza tangu atambulishwe Februari 4, 2025, ameongeza dozi ya mazoezi akiwahusisha wachezaji wote waliokuwa kwenye mpango wa mechi.
Leo imeshuhudiwa baada ya mechi dhidi ya JKT Tanzania kumalizika kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar kwa matokeo ya 0-0, wachezaji wote 21 waliokuwa katika mpango wa mechi wamefanya mazoezi katika makundi mawili huku wakionekana kuwa hoi baada ya kumaliza.
Kundi la kwanza lilihusisha wachezaji 15 waliocheza wakiwemo 11 walioanza na wanne waliotokea benchi wakitumia takribani dakika 15 huku wakipata muda wa kupumzika kidogo kila wanapomaliza zoezi moja na kupata wasaa wa kunywa maji.
Katika mazoezi hayo, walianza kuzunguka uwanja, kisha kukimbia mbio fupi kuanzia kati ya uwanja hadi golini. Baada ya hapo, wakanyoosha viungo na kwenda vyumbani tayari kwa kuondoka.
Wachezaji waliokuwa kundi la kwanza ni Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Hamad, Khalid Aucho, Clement Mzize, Mudathir Yahya, Prince Dube, Clatous Chama, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Stephane Aziz Ki, Kennedy Musonda na Duke Abuya.
Kundi la pili ni wale waliokuwa benchi ambao hawakucheza kabisa, nao walifanya mazoezi kwa takribani dakika 25, ikiwa ni muda mwingi zaidi kulinganisha na awali. Pia walikuwa wakipata muda wa kupumzika angalau dakika moja kila wanapohamia zoezi lingine na kunywa maji.
Katika mazoezi hayo yaliyoongozwa na Taibi Lagrouni, walianza kwa kuzunguka uwanja, kisha kuchezea mpira, ikifuatiwa kukimbia mbio fupi, kisha wakamalizia kwa kunyoosha viungo na kwenda vyumbani kubadilisha nguo.
Katika kundi hili waliohusika ni Aweso Aweso ambaye ni kipa chipukizi, nahodha Bakari Mwamnyeto, Kibwana Shomari, Nickson Kibabage, Shekhan Khamis, na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Mwanaspoti limeshuhudia mazoezi hayo ambayo wakati wachezaji wakiwa bize, benchi la ufundi lote la Yanga likiongozwa na Hamdi lilikuwa likifuatilia kwa umakini.
Mazoezi hayo baada ya mechi yamekuwa msaada mkubwa kwa Yanga kuongeza utimamu wa mwili kwa wachezaji hali iliyofanikisha kwa kiasi kikubwa timu hiyo msimu huu kucheza soka la kasi zaidi.
Gamondi alifanikiwa kuiongoza Yanga kucheza mechi 10 za ligi akishinda nane mfululizo kabla ya upepo kubadilika na kupoteza mbili mfululizo, akaondolewa.
Ramovic ndiye alifanikiwa kushinda mechi zote alizoongoza Yanga ambazo ni sita hadi anaondoka.
Kwa Hamdi, ameanza na suluhu, itakuwaje mbele ya safari katika kuhakikisha Yanga inatetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Yanga baada ya kumalizana na JKT Tanzania, Februari 14, 2025 itakaribishwa na KMC kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara mzunguko wa 19.