Mwalimu mkuu ahukumiwa kifungo kwa kuwapa majibu ya mtihani wanafunzi

Simiyu. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Sunzula B, Wilaya ya Itilima Mkoa wa Simiyu, Bahati Suguti amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh5 milioni kwa kosa la kufanya udanganyifu katika mtihani la darasa la nne mwaka 2023.

Katika kesi hiyo iliyotolewa hukumu leo Februari 2, 2025 na mahakama ya Wilaya ya Itilima, mahakama imewaachia huru washitakiwa wenzake watano ambao ni walimu baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.

Hii ni baada ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Robert Kaanwa, kueleza kuwa ushahidi uliotolewa unaonyesha washitakiwa hao watano ambao walikuwa ni wasimamizi wa mitihani, hawakuhusika kutenda kosa hilo.

Walimu walioachiwa huru na mahakama hiyo baada ya kutokuwepo ushahidi dhidi yao kulingana na hukumu hiyo ni Stephano Daud, Fauzia David, Mwita Boniface, Masatu Jepharine na Salome Aron.

Kulingana na ushahidi huo, mwalimu Suguti ambaye ametiwa hatiani, ndiye alikuwa akiwasaidia wanafunzi kwa kuwapatia baadhi ya majibu na hiyo ilibainika baada ya mitihani hiyo kusahihishwa na kuonyesha mfanano wa majibu.

Kwa mujibu wa ushahidi huo, mmoja wa walimu wasimamizi alifuatwa na mwalimu mkuu huyo ambaye alikuwa mshitakiwa namba moja, ili ampe ushirikiano lakini alikataa na hivyo ushahidi kumwelemea mwalimu huyo.

Ni kutokana na uzito wa ushahidi, Hakimu Kaanwa alisema upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha shitaka hilo pasipo kuacha shaka yoyote hivyo anatiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka mittatu au faini hiyo.

Awali kesi hiyo jinai namba 27062 ya mwaka 2024 ilikuwa ikiwakabilia walimu hao sita ambao walishitakiwa na makosa mawili ambayo ni moja ni kula njama ya  kutenda kosa pamoja na mbili ni kusaidia wanafunzi kutenda kosa la udanganyifu.

Katika hati ya mashitaka kabla ya kuachiwa kwa walimu watano, Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi,Jaston Haule alidai mahakamani kuwa walimu hao katika nyakati tofauti walitenda makosa hayo kinyume cha sheria.

Ilidaiwa kati ya Oktoba 25 na 26,2023, katika shule ya msingi Sunzula B, washitakiwa walidaiwa kula njama kinyume na kifungu cha 384 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika kosa la pili alidai katika tarehe hizo hizo kwenye mitihani ya upimaji ya darasa la nne ikiwa inaendelea washtakiwa waliwasaidia wanafunzi wa darasa la nne kutenda kosa la udanganyifu wa mitihani hiyo katika vyumba vya mitihani.

Kosa hilo lilikuwa ni kinyume na kinyume na kifungu 23 na 24 vya sheria NECTA sura ya 107 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2019 vikisomwa pamoja na kanuni ya 16(11)(c) za mitihani ya 2016 kama ilivyo tangazwa kwenye gazeti la serikali namba 89 la mwaka 2016.

Katika kesi hiyo jumla ya mashahidi tisa na vielelezo vinne vilitolewa na upande wa mashtaka, ambapo mahakama iliwakuta washitakiwa wote sita kuwa wana na kesi ya kujibu ndipo walitakiwa kujitetea ili kupangua tuhuma zinazowakabili.

Baada ya kujitetea washtakiwa wote, mahakama hiyo ikamtia hatiani mshtakiwa namba moja pekee na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini milioni tano. Suguti alipelekwa gerezani baada ya kushindwa kulipa faini.

Hukumu hiyo imekuja siku chache baada ya Katibu mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk Said Mohamed, kutangaza kuwafutia mitihani wanafunzi 100 waliofanya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne (SFNA) kutokana na udanganyifu.

Akitangaza matokeo ya mtihani huo Januari 4, 2025, Dk Mohamed alisema kati ya wanafunzi 100, wawili walifanya udanganyifu kwa kusaidiana ndani ya chumba cha mtihani, wanafunzi 98 walifanyiwa mitihani na wenzao wa darasa la tatu, tano na sita.

Related Posts