KOCHA Miloud Hamdi, amezionja dakika 90 za kwanza akiwa benchi akiiongoza Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliomalizika kwa matokeo ya 0-0, umepigwa Februari 10, 2025 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
Hamdi amerithi mikoba ya Sead Ramovic aliyeondoka Yanga Februari 4, 2025 baada ya mechi sita za ligi na kushinda zote.
Katika dakika tisini za kwanza kocha Hamdi kuiongoza Yanga baada ya ile ya kwanza kushuhudia akiwa jukwaani Uwanja wa KMC Complex walipotembeza kichapo cha 6-1 dhidi ya KenGold, kuna vitu ameonyesha mapema kama ndio tabia yake.

Kuna msemo wa Kiswahili unaobainisha kwamba ‘Tabia ya mtu ni kama ngozi, haijifichi.’ Hivyo basi kile alichokionyesha Hamdi dhidi ya JKT Tanzania ni wazi ndio tabia yake anapokuwa katika majukumu yake ya kufundisha.
Katika ufundishaji kila kocha ana mambo yake anayoyafanya ili tu kusaka pointi tatu.
Kwa Hamdi, ameonekana ni kocha asiyependa kukaa kwenye kiti wakati vijana wake wakivuja jasho kupambania pointi tatu.
Watangulizi wake, Miguel Gamondi na Sead Ramovic licha ya wao pia kuwa na tabia hiyo, lakini kuna wakati walikuwa wanakaa angalau dakika kadhaa kisha wanasimama. Kwa Hamdi, amesimama dakika zote tisini.
Gamondi alikuwa anasimama sana wakati wa mechi hasa zile kubwa dhidi ya Azam na Simba huku akitoa maelekezo lakini amewahi kukaa kwa muda kabla ya kuendelea na majukumu. Ramovic naye hivyohivyo.
Sasa Hamdi ambaye hakukaa hata mara moja wakati mechi ikiendelea ikimaanisha alisimama dakika zote tisini, alikuwa akibadili mikao ya kusimama tu.

Mbali na kusimama, pia alikuwa akitembea na matukio, timu yake ikishambulia anasogea upande ambao shambulizi limeenda kisha anarudi upande mwingine wakishambuliwa.
Kutokaa kwake kwenye mipaka iliyowekwa kuonyesha mwisho wa makocha kusimama na kutoa maelekezo, ilimfanya mwamuzi wa akiba (fourth official), Liston Hiyari wa Dar es Salaam mara kadhaa kwenda kumkumbusha mipaka yake.
2. UKIZUBAA KELELE ZINAKUHUSU
Kocha Hamdi hataki kuona mchezaji wake wakati mechi inaendelea azubae, anachotaka ni wote kuwa mchezoni.
Mara kwa mara alikuwa anamuita mchezaji aliyeonekana kama anategea na kumpa maelekezo. Baadhi ya wachezaji waliokutana na balaa hilo na Chadrack Boka na Djigui Diarra.
Ramovic alikuwa kocha mwenye mizuka iliyopitiliza lakini Hamdi, anayo kimtindo.
Alionekana katika matukio kadhaa ambayo wachezaji wake walipokosa nafasi za kufunga ikiwemo ile ya dakika 15 baada ya Pacome Zouzoua kupiga shuti lililoonekana linakwenda golini mwa JKT Tanzania lakini walinzi wawili walilala kwa pamoja kuuzuia mpira huo usipenye.

Pia shambulizi la Clement Mzize dakika ya 45 lililookolewa na kipa Yakubu Suleiman na kuwa kona, nalo lilimpa wakati mgumu kocha huyo mwenye uraia pacha wa Ufaransa na Algeria.
Si unafahamu viongozi wa benchi la ufundi Yanga wana sare maalum wanazovaa wakati wa mechi huku zikiwa na mdhamini wao mkuu ameandikwa kifuani? Sasa kwa Hamdi, siku ya kwanza kazini ametokelezea kibishoo.
Unaukumbuka ule wimbo wa wakali wawili Idrisa Makupula a.k.a Dira na Haashim Bakari a.k.a Taswira waliounda kundi la University Corner.
Wimbo huo si mwingine bali ni T-Shirt na Jeans. Verse ya pili kutoka kwa Dira inaanza kwa kusema; “Waone masistaduu au wacheki machizi, mtazame kidume halafu wacheki matozi, wamevaa tisheti na jeans wamenoga kichizi.”
Kiitikio kasimama Ferouz anakwambia; “Kila mmoja anapendeza (t-shirt na jeans), hakuna inayomchukiza (t-shirt na jeans), sitoweza kuiacha inanitoa chicha nami nawakilisha (t-shirt na jeans).”
Sasa basi kama wakali hao walivyotaja t-shirt na jeans ni mavazi ya mabishoo au matozi kwa wanaume na masistaduu upande wa wanawake, ndivyo alivyotokelezea kibishoo Kocha Hamdi.

Wakati viongozi wengine wa benchi la ufundi la Yanga wakiwemo makocha wasaidizi, madaktari na meneja wa timu wakivaa t-shirt nyeusi wengine za kijani huku chini wakipiga tracksuit na wapo waliovalia bukta nyeusi, Hamdi alipiga zake t-shirt na jeans zote rangi nyeusi kisha chini raba nyeupe.
Pigo zake za mavazi ni kama ilivyokuwa Ramovic ambaye naye alikuwa akivaa kibishoo sana.