Rais wa Marekani, Donald Trump, amesaini hati ya msamaha kwa aliyekuwa Gavana wa Illinois kwa tiketi ya Chama cha Democrat, Rod Blagojevich, almaarufu Blago, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 14 gerezani baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya kupokea rushwa.
Blagojevich aliondolewa madarakani mwaka 2009 na baadaye alikutwa na hatia mwaka 2011 kwa tuhuma za kupokea fedha ili kuuza nafasi katika Seneti iliyokuwa wazi baada ya Barack Obama kuchaguliwa kuwania urais mwaka 2008.
Akizungumza Ikulu baada ya kusaini hati ya msamaha, Trump alisema kuwa Blagojevich ameteseka kwa makosa makubwa ya ukiukwaji wa haki.
“Nafurahi kufanya hili nililolifanya. Nilikuwa nikimfuatilia, alitengenezewa tuhuma za uongo na kundi la watu wabaya, baadhi yao wakiwa ni wale ninaopaswa kushughulikia,” alisema Trump.
Katika muhula wake wa kwanza, Trump alimpunguzia adhabu Blagojevich, akidai kuwa alihukumiwa kimakosa, na kusababisha aachiwe kutoka gerezani mwaka 2020 alipokuwa akiendelea kutumikia kifungo chake akiwa nje.