Kabaisa na wenzake, waomba mahakama itoe maelekezo kwa Serikali

Dar es Salaam. Washtakiwa tisa wanaokabiliwa na kesi ya kusafirisha kilo 332 za Heroine na Methamphetamine, wameomba Mahakama itoa maelekezo kwa Serikali waongeze kasi ili upelelezi wa shauri hilo ukamilike kwa wakati.

Washtakiwa hao ni mvuvi wa samaki Ally Ally (28) maarufu kama Kabaisa, Bilal Hafidhi(31)ambaye ni mfanyabiashara; Mohamed Khamis (47) Mvuvi wa samaki na  Idrisa Mbona (33) ambaye ni  muuza magari.

Wengine ni Rashid Rashid (24) Beach Boy na mkazi wa Ubungo Maji; Shabega Shabega (24) mbeba mizigo na mkazi wa Saadan Kasulu.

Pia, yupo Dunia Mkambilah (52) ambaye ni mlinzi na mkazi wa Madale Kisauke;  Mfanyabiashara Mussa Husein (35) mkazi wa Mwambani na Hamis Omary (25).

Wakili wa washtakiwa hao, wamefikia hatua hiyo, baada ya Wakili wa Serikali Eva Kassa, kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumanne, Februari 11, 2025 kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Kassa amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, anayesikiliza kesi.

Kufuatilia hali hiyo, wakili wa washtakiwa hao, Hassan Rugwanya, ameieleza kuwa wateja wake wamekuwa ndani muda mrefu kutokana na mashtaka yanayowakabili hayana dhamana.

“Washtakiwa ni watuhumiwa na siyo wafungwa, hivyo tangu wameletwa Mahakamani hapa Aprili mwaka jana hadi sasa upelelezi bado,” amedai Wakili Rugwanya.

“Hivyo, tunaomba mahakama itoe maelekezo kwa upande wa mashtaka maana sioni kama tunaenda na spidi ya uboreshaji wa Hakijinai,” amedai wakili Rugwanya.

Akijibu hoja hiyo, wakili wa Serikali Kassa amedai hoja hiyo wataifikisha kwa mamlaka husika ili upelelezi ukamilike kwa haraka. Hakimu Mhini baada ya kusikiliza hoja hizo ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 20, 2025 kwa kutajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na kesi inayowakabili haina dhamana.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Aprili 16, 2024 karibu na Hotel ya White Sands, iliyopo wilaya ya Ilala, wanadaiwa kusafirisha kilo 100.83 za dawa aina ya Methamphetamine, kinyume na sheria.

Shtaka la pili, siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha kilo 232.69 za Heroine, kinyume cha sheria.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa Mahakamani hapo, April 22, 2024 wakikabiliwa na mashtaka hayo.

Related Posts