Hati chafu zatawala vyama vya ushirika Mara, RC aagiza Takukuru kuchunguza

Musoma. Asilimia 89 ya vyama vya ushirika mkoani Mara vilivyokaguliwa na Shirika la Usimamizi na Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (Coasco), vimebainika kuwa na hati zisizoridhisha katika kipindi cha mwaka 2022/23.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humo kuanza uchunguzi mara moja.

Mtambi amesema taarifa hiyo ya ukaguzi inaonyesha kuna viashiria vya ubadhrifu na matumizi mabaya ya mali za ushirika, jambo ambalo ni hatari kwa sekta ya ushirika ndani ya mkoa huo.

Mtambi ameyasema hayo leo Jumatano Mei 15, 2024 mjini Musoma alipokuwa anafungua mkutano wa Jukwa la Ushirika mkoani Mara.

“Taarifa hii inaonyesha hali sio nzuri kwenye sekta ya ushirika, mmesema wenyewe kuwa kuna baadhi ya viongozi wasiokuwa waadilifu wanatumia madaraka yao vibaya kwa maana wanatumia mali za ushirika kinyume cha utaratibu, hii haikubaliki lazima hatua zichukuliwe haraka sana kudhibiti hii,” amesema.

Mkuu huyo wa mkoa amesema miongoni mwa sababu zilizoifanya sekta ya ushirika kufa nchini kipindi cha nyuma ni pamoja na vitendo vya ubadhirifu na matumizi mabaya ya mali za ushirika na kwamba, Serikali haiko tayari kuona ushirika unakufa tena kutokana na vitendo hivyo ambavyo vinafanywa na viongozi wachache.

Amesema ustawi wa sekta ya ushirika una matokeo chanya katika suala zima la maendeleo endelevu katika jamii na nchi kwa ujumla.

Hivyo, amesema lazima sekta hiyo ilindwe kwa manufaa ya ustawi wa jamii nzima.

Mtambi amesema ili ushirika udumu na kuwa imara na kufikia malengo, uendeshaji wa vyama vya ushirika lazima ufanywe kwa kuzingatia sheria na taratibu.

“Natoa mwezi mmoja kuanzia sasa vyama vyote na wanachama wake wawe wamesajiliwa kwenye mfumo kama tume ya ushirika inavyoelekeza kwa sababu nimeambiwa hadi sasa usajili umefikia asilimia 65 pekee, viongozi simamieni hili,” amesema Mtambi

Akitoa taarifa ya hali ya ushirika mkoani Mara, Mrajisi Msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani humo, Lucas Kihondere amesema sekta hiyo inakabaliwa na changamoto kadhaa ikiwemo usimamizi mbovu wa baadhi ya viongozi.

“Ukaguzi uliofanywa na Shirika la Usimamizi na Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (Coasco) mwaka 2022/23 kwenye vyama 48 vya ushirika, ilibainika asilimia 89 ya vyama hivyo vilipata hati zisizoridhisha,” amesema Kihondere.

Amesema mkoa huo pia unakabiliwa na upungufu wa maofisa ushirika 12 huku halmashauri tatu zikiwa hazina kabisa, jambo linalo kwaza ukuaji wa sekta hiyo mkoani humo.

Amezitaja halmashauri hizo ni pamoja na ya Musoma Manispaa, Musoma vijijini na Butiama.

Meneja wa Chama Kikuu Cha Ushirika cha Wakulima Mkoa wa Mara (Wamacu), Samuel Marwa amesema upungufu wa maofisa hao unarudisha nyuma ustawi wa sekta ya ushirika mkoani humo.

“Kuna baadhi ya migogoro inasababishwa na upungufu wa maofisa ushirika ambao kama wangekuwepo wangesaidia kuondokana na hali hiyo, tunaomba maofisa hao wapatikane ili sekta hii iweze kuimarika zaidi kwa manufaa ya mkoa wetu,” amesema Marwa.

Related Posts