Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia dereva wa bajaji Ahmaded Kipozi (39) kwa madai ya ulevi uliomfanya asinzie na kupaki usafiri huo barabarani tukio lililosababisha foleni.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumanne Februari 11, 2025 na Kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, imeeleza dereva huyo ambaye pia hakuwa na leseni alifanya kosa hilo jana Jumatatu.
“Kikosi cha Usalama Barabarani kimemkamata Ahmaded Kipozi (39) mkazi wa Morogoro katika Barabara ya Morogoro-Dar es Salaam akiwa anaendesha bajaji bila leseni huku akiwa katika hali ya ulevi.
“Mtu huyo alibainika baada ya kukamatwa akiwa ameegesha bajaji yake katikati ya barabara na kusinzia kwa kuzidiwa na ulevi hivyo kusababisha foleni ndefu ambayo ilileta kero na taharuki kwa watumiaji wengine wa barabara. Alipimwa na kupatikana na ulevi kipimo 246.2mg/100ml,” amesema.
Aidha, jeshi hilo limesema taratibu za kisheria za kufikishwa mahakamani kwa dereva huyo zinaendelea.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo limemkamata Mwita Ally maarufu ‘Chinato’ (33), akiwa anaendesha gari namba T.458 BDB aina ya Suzuki Escudo kwenye eneo la Manispaa ya Morogoro akiwa katika hali ya ulevi.
“Baada ya kupimwa, Chinato amekutwa a kiwango cha ulevi 510.01mg/100ml, pia Lucas Beatus Lwehela (28), dereva wa gari la masafa marefu lenye namba za usajili T.117 EBK / T.817 EBL aina ya FAW akitokea nchini Rwanda kwenda Dar es salaam amekamatwa akiwa anayumbayumba barabaranio kiasi cha kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine.
“Baada ya kufanyiwa vipimo amepatikana na ulevi wa 431.3mg/100ml. Dereva huyu amekamatwa katika eneo la Mpange, Kijiji cha Wami Sokoine, Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro,”imeeleza taarifa hiyo