Manyara. Mkuu wa Wilaya ya Arumeru (DC), Amir Mkalipa ametumia mstari wa biblia kuwaomba wananchi walioandamana na kufunga barabara kwa zaidi ya saa nne kushinikiza Serikali kutatua changamoto zinazowakabili, kusitisha maandamano hayo.
Miongoni mwa changamoto hizo, ni kuwapo kwa eneo korofi linalosababisha mafuriko mara kwa mara, ambali limesababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.
Maji yanayosababisha maafa hayo yanatoka kwenye mito mitatu na kukusanyika sehemu moja, hivyo kusababisha mafuriko.
Kutokana na changamoto hiyo, wananchi walianza kufunga barabara saa 11 alfajiri hadi saa 2:44 asubuhi ya leo, Jumanne Februari 11, 2025, katika Kijiji cha Naisinyai, hali iliyomlazimu mkuu wa wilaya kufika kuwasihi wafungue barabara.
Wananchi hao kukata tatu za Kia (Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanajro), Majengo (wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha), na Naisinyai (Simanjiro, Mkoa wa Manyara), wamesema mafuriko katika mpaka wa kata hizo yamesababisha vifo na uharibifu wa mazao ya chakula.
Wamesema maandamano yao yamelenga kutoa ujumbe wa amani kwa mamlaka husika.
Akizungumza nao, DC Mkalipa ametumia mstari wa biblia: Wafilipi 4:13: “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu,” kuwaomba wananchi hao waliokuwa wamefunga barabara hiyo kutoka Mirerani kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).

Amesema amefika eneo hilo akiwawakilisha wakuu wa wilaya wenzake wa Arumeru na Hai ambao wako mkoani Dodoma kwenye majukumu mengine na kuwaomba wananchi hao kufungua barabara kuruhusu abiria waliokwama kuendelea na safari zao.
Mkuu wa wilaya amewahakikisha wananchi hao kesho Jumatano, Februari 12, 2025 kutafanyika kikao cha pamoja kati ya wakuu wa wilaya hizo tatu, madiwani pamoja na wenyeviti wa vijiji husika kwa lengo la kujadiliana na Bodi ya Bonde la Pangani na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhusu utatuzi wa tatizo hilo kabla ya mvua za masika hazijaanza.
“Nilikuwa DC Hai, hivyo hili tatizo nalifahamu na diwani alishakuja ofisini kwangu kuhusu suala hili, lazima tufike mwisho wa tatizo hilo, lengo lilikuwa ni kupeleka ujumbe na umeshafika, sasa tukatatue changamoto hii kama Serikali kabla mvua za masika hazijaanza,” amesema.
“Kwa sababu jamii ya kimasai ni jamii yenye heshima ni watu wema hawajawahi kuwa watu wabaya, nimeongea diwani kuanzia asubuhi saa 11 alfajiri, niwaombe sana hatuna sababu ya matumizi ya nguvu, nawaomba twendeni tukaangalie eneo, tuwache ndugu zetu halafu tupeane muda. Hata hela kama zipo, leo daraja haliwezi kujengwa na kuisha leo,” amesema.
DC Mkalipa amewaeleza wananchi hao hakuna atakayepata shida lakini busara na heshima ni muhimu hasa kwa viongozi ambao wameonyesha kujali na kuwa watachukua juhudi kuhakikisha tatizo hilo linaisha kabisa.
“Kwenye bajeti unaweza ukasema tunaliondoa tatizo kiasi hiki, lakini kwa maana nyingine ni kuliondoa kabisa tatizo, ndiyo maana mwanzo nilisema “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu, haleluya….Mzee (Diwani) si nimekupigia saa 11 alfajiri? alihoji DC Mkalipa.

Baada ya kuzungumza na wananchi hao kwa zaidi ya dakika 10, Mkalipa ameongozana na madiwani, wenyeviti na mamia ya wananchi hao kukagua maeneo hayo yenye changamoto ili watakapokaa kikao kesho wajue pa kuanzia.
“Leo tufanye kazi kubwa na nyie tukague tatizo linapoanza hadi linapoishia, kesho tukae kikao kwa sababu pia hatuwezi kukaa saa 24 hapa, lazima barabara hii itumike kwa ajili ya wananchi, inawezekana kuna mgonjwa au kuna msafiri isingekuwa busara kuendelea kukaa hapa,” amesema.
Awali kuanzia saa 11 alfajiri wananchi hao waliokuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali wakiwa wameshika matawi ya miti kuashiria amani, walifunga barabara hiyo.
Licha ya viongozi wakiwemo madiwani, wenyeviti wa vijiji na askari polisi kuwataka waondoke na kusubiri viongozi nje ya barabara, wananchi hao waligoma kuwasikiliza viongozi hao hali iliyosababisha polisi kuongezeka katika eneo hilo.
Mmoja wa wananchi hao, Petro Laizer amesema kilichowasukuma kufunga barabara hiyo ni mafuriko ya mara kwa mara ambayo yamesababisha ndugu zao kufariki na mashamba yao yakiharibiwa.
Naye Isack Kitwana kutoka Kijiji cha Naisinyai, amesema kwa kipindi cha miaka mitano wamekuwa wakiteseka na kwa tatizo hilo na viongozi wamekuwa wakifika eneo hilo bila utatuzi wa kudumu.
“Viongozi wa mikoa mitatu tunawataka hapa waje hapa tulishadanganywa zaidi ya miaka hiyo mitano, wamekuja kutembelea hapa na tathmini ya gharama walishakuja kufanya ila maji yanaongezeka, waje hapa tusikilizwe, hata kama wapo Ulaya waje,” amesema
Diwani wa Majengo, Benard Kivongo amesema wananchi hao wamefikia hatua hiyo kutokana na suala hilo kuwa la muda mrefu bila utatuzi wa kudumu.
Diwani wa Naisinyai, Taiko Laizer amesema suala hilo linapaswa kuangaliwa kwani jamii hiyo siyo ya wababishaji ila wamechoka.