Lisbon. Mtukufu Mwanamfalme Rahim Aga Khan V ametawazwa rasmi kuwa kiongozi wa jamii ya Ismaili na Imam wa 50, kwenye hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa jamii ya Waislamu wa Shia Ismaili duniani.
Hafla hiyo imefanyika leo Februari 11, 2025 katika ofisi kuu ya kiutawala ya Imam inayofahamika kwa jina la Diwan ya Ismaili Imamat iliyopo jijini Lisbon nchini Ureno.
Kwenye hafla hiyo viongozi wa jamii ya Ismaili wameahidi utii wa kiroho kwa Imam wa 50 wa kisheria kwa niaba ya jamii ya Ismaili duniani.
Waismaili kutoka duniani kote walishuhudia hafla hiyo ilioonyeshwa mubashara kwenye mtandao katika Jamatkhana zao (sehemu za kukusanyika) katika nchi zaidi ya 35 duniani.
Mtukufu Aga Khan kwenye hotuba yake ametoa heshima na neno la shukrani kwa baba yake mpendwa, marehemu Prince Karim Aga Khan IV, na ameishukuru familia yake kwa uwepo wao na msaada wao.

Pia, amezishukuru serikali za Ureno na Misri kwa namna walivyokubali michango ya baba yake na kuwezesha mipango ya heshima kwa mazishi na maziko yake.
Hotuba ya Mtukufu Aga Khan V kwa jamii ya Waismaili duniani ni ya kwanza tangu ashike wadhifa huo baada ya kifo cha baba yake Mtukufu Aga Khan IV aliyefariki dunia Februari 4, 2025, jijiji Lisbon nchini Ureno na alizikwa Februari 9, 2025, katika mazishi ya faragha yaliyofanyika kwenye mji wa Aswan, nchini Misri.
Katika hotuba yake hiyo ameahidi kujitolea maisha yake kwa ajili ya huduma ya kiroho na kimaisha ya jamii ya Jamat ya Ismaili.
Amezungumzia misingi ya imani ya Kiislamu ya Ismaili kuwa ni umuhimu katika kuweka usawa kati ya mambo ya kidunia na ya kiroho, na kuitekeleza Imani kwa vitendi mara kwa mara.
Ujumbe wake ulilenga dhana za kimataifa ya amani, uvumilivu, jumuishi na msaada kwa wenye uhitaji.

Ameitaka jamii yake kuwa raia wema na wenye kujishughulisha kwenye nchi wanazoishi na kuwa jamii ya mfano kwenye masuala yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi.
Akiwa mshiriki mkubwa katika kazi za Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan kwa miongo kadhaa, Mtukufu Mwanamfalme Rahim Aga Khan V ameahidi kuendeleza kwa usawa shughuli za mtandao.
Pia, ameahidi kudumisha uhusiano wa kirafiki na Serikali na washirika ikiwamo kufanya kazi nao kwa karibu, kama alivyofanya baba yake, kwa ajili ya amani, utulivu na fursa.
Hafla hiyo ya kupewa mamlaka ilihusisha usomaji wa kidini, utoaji na kuvaa mavazi yanayoshairia kushika ofisi, na ahadi ya kiroho ya utii kutoka kwa viongozi wa jamii ya Ismaili kwa niaba ya Waismaili wote duniani.
Pia, ni desturi kwa Imam kutoa hotuba kwa jamii yake katika tukio hili. Hafla hiyo inathibitisha mamlaka ya Imam kama kiongozi wa kiroho wa sasa, mwenye uhai, wa jamii ya Waismaili wa Kishia duniani.