Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema mpango wa kukagua magari kwa macho sasa basi, badala yake magari yote zitatakiwa kukaguliwa kila mwaka kitaalamu kupitia kituo cha ukaguzi ambacho kina ubora duniani na kupunguza ajali barabarani.
Dk Mwinyi ameeleza hayo leo Jumanne, Februari 11, 2025 wakati akifungua kituo cha kisasa cha ukaguzi na upasishaji wa vyombo vya moto Dole Unguja.
Amesema sema hatua hiyo ni muhimu katika kuboresha mfumo wa ukaguzi wa magari Zanziba na itasaidia kuongeza usalama barabarani, kupunguza ajali, na kuhakikisha vyombo vya moto vinakuwa katika hali nzuri.
“Kutumia vituo vya ukaguzi vya kiwango cha kimataifa, Zanzibar inajiweka katika nafasi nzuri ya kufuata viwango bora vya kimataifa, na kuleta ufanisi zaidi katika sekta ya usafiri wa barabarani,” amesema.
Kuwapo kwa kituo hicho kwa mujibu wa kiongozi huyo, kitafungua ukurasa mpya katika jitihada za serikali za kuimarisha usalama kwa watumiaji wa barabara kwani imekuwa ikichukua hatua za makusudi za kuhakikisha usafiri wa barabarani unakuwa salama muda wote ili kupunguza ajali.

Miongoni mwa hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa ni pamoja na kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya barabara Unguja na Pemba kwa kuweka njia za watembea kwa miguu, alama za usalama, taa, vituo vya daladala na kuweka sehemu maalum kwa ajili ya maegesho ya magari.
Alisema pia Serikali imenunua vifaa kwa ajili ya kupima ulevi wa madereva na mifumo ya utoaji leseni utakaowezesha kuwapata madereva bora wenye ueledi na watakaojiepusha na makosa ya barabarani pamoja na kuweka miundombinu kwa watu wenye mahitaji maalum.
Ametumia fursa hiyo kuwataka madereva kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa vyombo vyao ili kuzuia ajali za barabarani na kuimarisha usalama wa brabarani kwa ujumla.
“Sasa madereva wanaweza wakaweka miadi kwa njia ya simu bila ya kukaa foleni na chombo chake kitakaguliwa ndani ya dakika 15 haya ndio mambo tunayoyataka katika nchi yetu, mambo ya kisasa tuendane na sasa uliokuwepo duniani,” amesema
Dk Mwinyi alisema serikali inandelea kufanya marekebisho ya sheria ya usafiri barabarani pamoja na kanuni zake ili kuhakikisha kunakuwa na huduma bora ya usafiri wa barabara ambazo ni salama kwa watumiaji wote wakiwemo wazee na watu wenye mahitaji maalum.
Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha huduma za usafiri hapa Zanzibar ambapo mbali na ujenzi wa kituo hicho pia imepanga kuanzisha hudumza za usafiri wa umma kwa kutumia mabasi ya kisasa katika mji wa Zanzibar.
Vituo vya kisasa vya mabasi vinatarajiwa kujengwa Chuini, Malindi, Mwera, Jumbi, Mwanakwerekwe, Buyu, Fumba na vingine tayari kimoja kimejengwa Kijwangani.
Alimpongeza mwekezaji mzalendo kampuni ya Zenj Merchandise kwa kushirikiana na serikali kuimarisha huduma za usafiri na inathamini mchango wake na kuahidi kutoa ushirikiano ili kuona mradi huo unapata mafanikio.
Aliiagiza Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani, Jeshi la Polisi na Kikosi cha Usalama Barabarani kuongeza nguvu katika kusimamia sheria za usafiri barabarani na kutoacha kuchukua hatua kwa dereva yoyote atakaekiuka kutii sheria zilizopo.
“Ni lazima tuwe na jitihada za pamoja katika kuhakikisha nchi yetu inakabiliana na makosa ya barabarani ambayo yamekuwa yakiongezeka na kusababisha athari kubwa ikiwemo vifo, ulemavu na uharibifu wa mali,” alisisitiza.
Mapema Mwekezaji wa kituo hicho, Taufik Salum Turkey amesema Kampuni ya Zenj Merchandise ni kampuni pekee ndani ya bara la Afrika iliyoshirikiana na kampuni tatu ya ukaguzi zinazojulikana duniani kote.
Amesema kampuni kama Maha inazalisha mashine ambazo ni za kwanza duniani, wakaguzi wa masuala ya barabarani ikiwemo kampuni namba moja ya Kijerumani DKT ipo Zanzibar na kampuni ya Applus kutoa mafunzo kwa vijana ambao wataweza kuajiriwa duniani wakishapata cheti.
Alisema lengo la kutengeneza kituo hicho pia kitatoa mafunzo kuona vijana wanapata ujuzi wa kufanya ukaguzi na kuweza kuajiriwa Zanzibar, Tanzania Bara, Afrika na duniani kote.
Akitoa taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk Habiba Hassan Omar, alisema ujenzi wa kituo hicho ulianza Agosti 2024 na kukamilika Febuari 2025.
Alisema mkandarasi wa kituo hicho ni Kampuni ya Yamar Bulding Contractions chini YA msimamizi Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) ambapo mradi huo hadi kukamilika kwake umetumia zaidi ya Sh2.8 bilioni ambazo zimetolewa na mwekezaji.
Alifahamisha kuwa kituo hicho kina ukubwa wa mita za mraba 2,940 na kina uwezo wa kuhudumia zaidi ya vyombo vya moto 350 kwa siku moja.
Alisema kituo hicho kimefungwa laini sita za ukaguzi na kila laini moja ina vituo vinne vya ukaguzi na kina uwezo wa kupima mwendo, breki, moshi, taa za vyombo na chombo chochote kinachotembea barabarani kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.